Mtoki au kwa lugha ya kitaalamu, swollen lymph nodes or glands, ni uvimbe wa tezi unaojitokeza katika mwili wa mtu baada ya mwili kuumia na kushambuliwa na vijidudu au bakteria wasababishao magonjwa au wavurugao utendaji kazi wa kawaida wa mwili.
Tezi hizi (lymph nodes/glands) zinapatikana sehemu mbalimbali katika mwili, na kazi zake maalumu ni kugundua na kushambulia vitu au wadudu mbalimbali wanaoingia katika mwili na kusababisha magonjwa, hivyo ni kitu muhimu sana katika ulinzi au kinga ya mwili. Miongoni mwa sehemu katika mwili ambapo tezi hizi hupatikana ni maeneo ya nyonga (groin), nyuma za masikio, chini ya taya na kidevu, nyuma ya kichwa, maeneo ya kwapani (armpit) na shingoni.
Mara nyingi vitu vinavyosababisha mtu apate mtoki ni pamoja na mtu kupata maambukizi ya magonjwa mfano ugonjwa wa vidonda koo au tonsillitis, lakini mbali na maambukizi pia mtu anaweza kuwa kaumia sehemu ya mwili mfano mguuni kapata kidonda, ingawaje kupata mtoki SIYO lazima uwe na kidonda, mtu pia anaweza kupata mtoki kutokana na mambo ya kinga ya mwili kutokuwa katika hali nzuri, mfano endapo mtu ana ugonjwa kama vile ugonjwa wa joints za vidole vya mikononi na miguuni, Rheumatoid Arthritis, au endapo mtu ana upungufu wa kinga mwilini, UKIMWI, anaweza kupata mtoki, pamoja na hayo inawezekana mtu akawa na matatizo ya damu, kansa ya damu, leukemia, pia anaweza kupata mtoki.
Dalili za mtoki ni pamoja na maumivu sehemu yenye tezi, mfano inawezekana ikawa ni kwapani, katika nyonga au shingoni, mtu anaweza kupata homa, sehemu husika inaweza kuwa nyekundu (hii ni kutokana na kuongezeka kwa mtiririko wa damu katika sehemu hiyo).
Katika hali ya kawaida ni vigumu kuweza kuishika sehemu ya mwili na kuihisi tezi, hii ni kutokana na udogo wake, ina umbo la punje ya haragwe na ukubwa wake ni kitu kisichozidi inch moja. Endapo mtu kapata maambukizi au kaumia au kapata kitu chochote kile kinachoweza kuifanya tezi ivimbe, ndipo mtu utakapoweza kuishika sehemu husika na kuweza kuihisi tezi katika mwili wako.
Mtoki unaojitokeza ghafla na unakuwa na maumivu mara nyingi husababishwa na kuumia sehemu ya mwili au mwili kupata maambukizi fulani mfano vidonda kooni, tonsillitis.
Kutegemeana na historia ya mgonjwa au mtu mwenye uvimbe huu, daktari atapendekeza aina fulani ya vipimo vifanyike ili kuweza kutoa mwangaza wa tiba gani uweze kupewa. Kuna baadhi kama nilivyokwisha kueleza hapo awali kuwa chanzo inawezekana kikawa ni maambukizi ya vijidudu mfano bakteria, hivyo daktari atafanya maamuzi ni kundi lipi la dawa (antibiotics) litafaa kulingana na hali yako, pia kuna wengine wanao uvimbe ambao hauna maumivu na pengine ukubwa wake unaongezeka siku hadi siku, hapa pia inawezekana kikawa ni kitu kingine na baada ya vipimo vya kutosha huduma sahihi inaweza kutolewa.
Mpenzi msomaji, makala hii nimeiandika ili kukushirikisha mawazo kuhusu kile unachokifahamu kuhusu mtoki, na siyo njia mbadala ya kukufanya usifike katika wataalamu wa afya endapo utakuwa na tatizo hili, fika kwa wataalamu walio karibu nawe ili kuweza kujua namna bora zaidi ya kukusaidia.
Chanzo: Tanzlife Company Limited
Pingback: MTOKI, MAANA YAKE, VISABABISHI, DALILI ZAKE, UGUNDUZI PAMOJA NA MATIBABU YAKE - Blog Mama | Blog Mama