Hali ya mwili au sehemu ya viungo katika mwili kujaa maji na kuwa na muonekano kama vile uvimbe kitaalamu hujulikana kama Edema.
Vipo vitu au sababu mbalimbali zinazopelekea mwili au sehemu ya viungo katika mwili zijae maji. Sababu hizo ni pamoja na, magonjwa ya moyo ( congestive heart failure ) ambapo kutokana na moyo kushindwa kufanya kazi zake vizuri, husababisha damu ishindwe kufika katika viungo vingine vya mwili mfano miguuni. Hii itasababisha mwili ukusanye au uhifadhi maji mengi zaidi ya mahitaji halisi na matokeo yake husababisha mwili uwe kama umevimba.
Matatizo ya Aleji ( Allergic Reactions ). Inawezekana mwili umepatwa na chembe chembe ambazo haziendani na muundo mzima wa mwili, mfano wa chembe chembe hizi ni vyakula, mafuta ya kujipakaa au hata sumu baada ya kung’atwa na mdudu. Hivi vyote huweza kukusababishia mwili ujae maji haya ambayo huwa na muonekano wa uvimbe katika sehemu husika ya mwili.
Magonjwa ya ini ( liver cirrhosis ), ambayo hupunguza utendaji kazi wa ini ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa vitu muhimu vinavyopatikana katika damu mfano protin (albumin).
Upungufu wa protini mwilini unaoweza kusababishwa na matatizo ya kuwa na lishe duni au magonjwa ya ini.
Magonjwa ya figo. magonjwa ya figo hupunguza utengenezaji wa damu mwilini kutokana na kuathiriwa kwa vitu muhimu katika figo vinavyohusika na damu ( erythropoietin ).
Inawezekana mtu mwili wake ukajaa maji kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya mwili, mfano ni wamama wajawazito ambao baadhi yao huwa wanavimba miguu kutokana na miili yao kuwa na ongezeko la mahitaji ya damu ili kuweza kuutoshereza mzunguko mzima hadi kufika kwa kiumbe/viumbe walioko tumboni.
Mpenzi msomaji, baada ya kufahamishana miongoni mwa mambo yanayoweza kupelekea mtu apate hali hii ya mwili kujaa maji pia ni vyema kujua namna ambavyo maji haya hujitokeza na kusababisha muonekano wa uvimbe.kwa mfano, ni kwa nini unapong’atwa na mdudu ndiyo uvimbe unajitokeza?, nini kinatokea katika mwili wako hadi ngozi inajaa au kuvimba?. Katika mfano huo ngozi hujaa maji au kuvimba baada ya uwezo wa mishipa ya damu kuruhusu maji kupita ( permiability ) kubadilika ambapo mishipa hii ya damu huruhusu maji mengi zaidi yapite au yahame kutoka katika mchanganyiko wa damu na kuhamia katika tishu au nyama za mwili nje ya mishipa ya damu. Maji haya kwa kuwa hayapo katika mishipa basi husababisha sehemu hiyo ya mwili iwe kama imevimba, ila kwa upande wa pili hali hii huruhusu pia kinga za mwili au seli zinazohusika na ulinzi wa mwili zifike kwa wingi zaidi katika sehemu hiyo (mfano ulipong’atwa) na kuweza kupambana ili kuziwezesha seli hizo zirejee katika utendaji kazi wake wa kawaida, kwani maji hayo huwa na kiwango kikubwa cha seli zinazo ulinda mwili ambazo ni seli hai nyeupe za damu ambazo kitaalamu huitwa leucocytes.
Mambo niliyoyaeleza hapo juu ni baadhi tu ya yale yanayoweza kumfanya mtu mwili wake ukajaa maji na hivyo kuonekana kama umevimba. Endapo mtu atakuwa na tatizo hilo mara nyingi utatuzi au matibabu yake yanategemeana na kisababishi cha hali hiyo ni nini, hivyo matibabu hutofautiana. Endapo unatatizo hili fika katika kituo cha kutolea huduma za afya kilicho karibu na wewe ili uweze kupata huduma zinazostahili mapema.
Chanzo: Tanzlife Company Limited
Pingback: VIUNGO AU MWILI KUJAA MAJI ( EDEMA ) | Blog Mama