Articles

UTUMIAJI WA VINYWAJI MBALIMBALI KATIKA KUMEZA DAWA

By

on

Matibabu ya magonjwa mbalimbali yamejikita katika vipengele vya ushauri, mazoezi, matumizi ya dawa, lishe pamoja na vitu vingine kwa kadri itakavyoonekana inafaa, lakini kikubwa ni kulingana na ugonjwa au tatizo ambalo mtu analo.

Katika matumizi ya dawa, kutegemeana na aina ya dawa pamoja na hali ya mgonjwa, dawa inaweza kutumika kupitia njia mbalimbali kama vile njia ya sindano, kinywa (Kumeza), kupakaa, kunusa au hata kuweka au kupandikiza katika sehemu ya mwili.

Mpenzi msomaji, leo nimeona ni vyema kubalidishana uzoefu nanyi kuhusiana na matumizi ya dawa kupitia njia ya kinywa(kunywa/kumeza/kulamba). Hii ni njia mojawapo ambayo watu wengi  wamewahi kuitumia katika kupata matibabu yao pindi walipokuwa na tatizo la kiafya.

Zipo sababu za msingi zinazoweza kupelekea mtu apate matibabu kupitia njia hii, kwanza ni njia rahisi kwa mtu kuitumia hata anapokuwa mbali na mtaalamu wa afya au daktari, pili haihitaji vifaa vingi vya kitaalamu ili kuwezesha dawa kutumika, ni njia isiyosababisha maumivu katika mwili wa mtumiaji mfano sindano huleta maumivu.

Ili dawa iweze kutumika kwa njia ya kinywa, itahitaji viwezeshi ili dawa iweze kumezeka kwa urahisi. Mfano wa viwezeshi hivyo kwa ilivyozoeleka na wengi ni maji ya kunywa. Lakini je, umezaji wa dawa ni lazima uende sambamba na maji ya kunywa?, vipi kuhusu maziwa?, je habari ya juisi, chai, soda na maji ya limao je?.

Mpenzi msomaji jambo ambalo unapaswa kulifahamu na kulikumbuka ni kwamba, dawa pia zina tabia za asili ambazo huziwezesha  kuyeyuka katika mazingira ya aina Fulani pindi zinapokuwa zimetumika. Tabia hiyo ya dawa inahusika na uyeyushaji, solubility.

Kulingana na aina ya dawa pamoja na chembechembe zilizomo katika dawa, uyeyukaji wa dawa unaweza kuwa mzuri katika maji, dawa nyingine huyeyuka vizuri katika mafuta, nyingine katika kimiminika chenye uchachu, acid, na kadharika. Sifa hizi ndizo zinazopekelea mtu ashauliwe kumeza dawa kwa msaada wa kunywa maji au kimiminika kingine.

Pamoja na dawa nyingi kushauriwa au kuzoeleka kutumiwa pamoja na maji ya kunywa, pia zipo dawa ambazo ili ziweze kuyeyuka tumboni kwa urahisi na kuanza kufanya kazi mapema zinahitaji mazingira yenye uchachu (Acid) na pia mafuta.

Dawa zinazohitaji mazingira yenye mafuta ili ziweze kuyeyuka kwa urahisi tumboni, maana yake ni kwamba dawa hizo zinaweza kumezwa kwa msaada wa kimiminika chenye mafuta (Mfano maziwa, baadhi ya dawa za kutibu Malaria), au kula vyakula vyenye mafuta ili tumboni dawa iweze kuyeyuka kwa urahisi. Pia dawa zinazohitaji mazingira yenye uchachu au acid, maana yake ni kwamba zinaweza kumezwa kwa kutumia kimiminika chenye uchachu mfano juisi, au hata maji ya limao au machungwa  (Mfano wa dawa ni baadhi ya dawa za kuongeza damu).

Tabia hizo za dawa zinaturahisishia kutambua kuwa ni vyakula vya aina gani au ni vimiminika vyenye sifa zipi vinapaswa kutumika pindi swala zima la matibabu na umezaji wa dawa unapofika. Pia, ni msaada kutambua aina ya kimiminika kinachopaswa kutumika pindi tatizo la matumizi yasiyokuwa salama ya dawa (kuzidisha dozi) yanapojitokeza. Mfano endapo dawa huyeyuka kwa urahisi katika mafuta, haitokuwa salama zaidi kumpatia mtu maziwa ili kumsaidia, kwani maziwa yana mafuta na yataiwezesha dawa hiyo kuyeyuka kwa urahisi zaidi na hivyo kushindwa kumsaidia mgonjwa.

Pamoja na mambo mengine ya msingi ambayo mtaalamu wa afya atakufahamisha kuhusu matumizi ya dawa aliyokupatia, miongoni mwa maswali ambayo unapaswa kukumbuka kumuuliza mtaalamu ni hili, je, katika kutumia dawa hii ninapaswa kutumia vyakula vya aina au asili gani, na pia vipi kuhusu vinywaji?. Yote hayo ni katika kurahisisha matibabu yako na kuwa na tahadhari endapo tatizo lolote litajitokeza.

Mpenzi msomaji, dawa yoyote inaweza ikawa sumu, tumia dawa kulingana na ushauri fasaha unaopewa na wataalamu wetu.

Chanzo: Tanzlife Company Limited 

About Admin

Avatar

Recommended for you