Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zinakabiliwa na changamoto ya vifo vya watoto wachanga na wenye umri chini ya miaka mitano.
Licha ya vifo vya watoto pia Tanzania inakabiliwa na changamoto ya vifo vya kinamama wajawazito ambapo inaelezwa katika kila wanawake 100,000 vifo ni 454.
Kulingana na takwimu za kitaifa vifo vya watoto vimepungua kutoka 147 mwaka 1999 hadi kufikia vifo 81 kwa kila watoto 1000 waliozaliwa hai huku vifo vya watoto chini ya mwaka mmoja vikiwa vimepungua kutoka 99 hadi kufikia 51.
Licha ya juhudi zinazofanywa na serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo bado takwimu za vifo hivyo hapa nchini si nzuri hivyo kunahitajika hatua za makusudi za kuhakikisha vifo hivyo zinapungua ama kuondoka kabisa.
Ziko sababu kadhaa zinazosababisha vifo hivyo zikiwemo umaskini, matatizo ya uzazi, lishe duni, magonjwa,baadhi ya wazazi na walezi kutokuwa makini katika malezi ya watoto wao, upungufu wa watumishi katika sekta ya afya, upungufu wa vifaa tiba na madawa na huduma duni za afya katika baadhi ya maeneo .
Vifo hivyo vimesababisha kurudisha nyuma gurudumu la maendeleo kwani baadhi ya familia zimekuwa zikitumia muda mwingi kupata suluhu ya matatizo hayo huku serikali nayo ikijikuta ikitumia gharama kubwa kutibu.
Wakati wa ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo jijini Dar es Salaam, Rais Jakaya Kikwete alishtushwa na takwimu za vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Kwa Mkoa wa Dar es Salaam takwimu za vifo hivyo zinaonyesha kuwa ni 83 katika kila watoto 1000 hali ambayo ilimshangaza rais Kikwete kutokana na kutofautiana na maeneo mengine hasa ya vijijini ambako kuna changamoto nyingi lakini idadi ya vifo hivyo iko chini.
Rais Kikwete alishtushwa na takwimu hizo kwa jili la Dar es Salaam ambalo kwa kiasi kikubwa huduma na kampeni ziko juu ukilinganisha na maeneo mengine ya vijijini.
Baadhi ya watendaji walijitetea kuwa wamejitahidi kupunguza vifo vya wanawake wajawazito lakini bado inawezekana kupunguza pia vifo vya watoto kwa kuwepo mikakati madhubuti itakayoonekana kimatendo.
Ingawa Rais Kikwete pamoja na mambo mengine alishauri kujengwa kwa hospitali maalum za wazazi lakini pia kuna haja ya kuwepo kwa ushirikiano wa karibu baina ya viongozi wakuu na watumishi wa afya bila ubaguzi kwani hali hiyo itasaidia watoa huduma kutoa huduma bora za afya ikiwa ni pamoja na kuwa na motisha yaani posho ya mazingira magumu ya kazi.
Pia ziwepo jitihada za kuwahamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa bima ya afya ili kupunguza matatizo ya matibabu kwa wananchi kwa sababu baadhi ya watu wamekuwa wakishindwa kupata huduma sahihi za afya kutokana na kutokuwa na pesa.
Kwa watumishi walioko maeneo ya vijijini kuwe na mkakati wa kuhakikisha wanaboreshewa mazingira yao kama vile kuweka umeme wa jua kwenye vituo na nyumba za watumishi na kubuni mbinu nyingine ili kusaidia watumishi wanaoishi maeneo ya pembezoni.
Jitihada nyingine ni kuhimiza matumizi ya chanjo dhidi ya kujikinga na magonjwa mbalimbali kama vile kifua kikuu, polio, dondakoo, pepopunda, kifaduro, homa ya ini, homa ya uti wa mgongo, surua, vichomi na nimonia.
Tanzania kama nchi nyingine zinazoendelea inatakiwa kufanya juhudi kubwa ili kufikia malengo ya nne na tano ya milenia ifikapo mwaka 2015 ambayo yanaelekeza kupunguza vifo vya watoto walio na umri chini ya miaka mitano. Pia jamii inatakiwa kuwezeshwa kuibua matatizo na kuweka afya ya uzazi na mtoto katika mipango yao ya maendeleo.
Chanzo: Tanzlife Company Limited