Kuna msemo unaosema kuwa, “Afya ni mtaji”, ukiwa na maana kuwa, mtu unapokuwa na afya nzuri ni tayari unakuwa na uwezo wa kufanya au kujihusisha na kazi tofauti tofauti katika jamii na kupata matokeo yenye ufanisi, kwani mwili wako, akili na roho yako vipo katika hali ya uimara wa kutosha.
Kwa sababu ambazo yawezekana zikawa ndani au nje ya uwezo wa mtu, wengi wetu tunajisahau kuwa, bila kuwa na afya imara hakuna kitu ambacho mtu utaweza kukifanya kwa ufanisi. Badala yake tumekuwa tunafanya kazi zetu za kila siku bila ya kuzingatia au kuchukua tahadhari dhidi ya hatari za kiafya zinazoweza kumpata mtu kutokana na mazingira ya kazi anazozifanya.
Mazingira ya kazi hutofautiana kwa mtu na mtu, pia hatari za kiafya zinatofautiana kwa kazi na kazi.
Ni wewe ndiye unayefahamu kuwa unafanya kazi zako katika mazingira gani, ila inawezekana ukawa hujafahamu kuwa mazingira ya kazi zako yana hatari zipi za kiafya, au unazifahamu hatari za kiafya ila hufahamu njia salama zaidi za kujilinda dhidi ya hatari hizo.
Kutokana na kazi tunazozifanya kila siku, baadhi ya vitu ambavyo vinapatikana katika mazingira ya kazi ambavyo ni hatari kwa afya zetu ni kama vile, vumbi (la vyuma, mbao) kemikali mbalimbali, joto (la jua, moto), bacteria (zaidi sana sehemu za kutolea huduma za afya), kutokana na aina ya kazi inawezekana ukaufanyisha mwili kazi kubwa zaidi kuliko uwezo wake, hatari za kuumia, kupata msongo wa mawazo na kuumia kisaikolojia na pia inawezekana mazingira ya kazi yakakufanya mwili wako usichangamke. Hivyo ni baadhi ya vitu au mazingira ya kazi ambayo tunatakiwa kuyachukulia tahadhari ili tuendelee kuzilinda afya zetu.
Miongoni mwa magonjwa ambayo mtu anaweza kuyapata kwa kutegemeana na mazingira ya kazi ni kama vile, magonjwa ya mapafu ikiwemo kansa, kansa za ngozi, magonjwa ya akili, upofu, magonjwa ya moyo na kisukari pamoja na kulemaa viungo vya mwili.
Baadhi ya tahadhari ambazo tunaweza kuzichukua ili kujilinda na tuweze kuendelea kufanya kazi katika hali ya usalama wa afya zetu zaidi ni kama vile, kuzingatia mavazi ya kazi (mfano katika ujenzi, migodi, mashambani au viwandani), kupata chanjo au dawa kutegemeana na aina ya vijidudu hatarishi, kufanya mazoezi (kuuchangamsha mwili ili kuepukana na hatari ya kupata magonjwa ya moyo na kisukari, kuichangamsha akili), kuuruhusu mwili upumzike, pia ni vyema ukaonana na mtu mwenye utaalamu zaidi ili akushauri endapo kuna jambo ambalo linakutatiza ili uweze kujilinda ipasavyo.
Kumbuka ya kuwa, mtu wa kwanza mwenye wajibu wa kuilinda afya yako, ni wewe mwenyewe. Chukua muda wa kutafakari kuwa, unafanya kazi katika mazingira gani, kisha chukua hatua za kuilinda afya yako ili kazi yako uweze kuendelea kuifanya kwa ufanisi zaidi.
Chanzo: Tanzlife Company Limited