Sikio ni kiungo muhimu katika mwili wa binadamu, humuwezesha mtu kupata mawasiliano na kuelewa nini kinaendelea katika mazingira aliyopo.
Sikio limegawanyika katika sehemu kuu tatu, kuna sehemu ya ndani (Inner Ear), sehemu ya kati (Middle Ear) na pia kuna sehemu ya nje (Outer Ear). Kila sehemu katika sikio ina kazi zake maalumu, ila kwa mada ya leo tutazungumzia sehemu inayohusika sana na uwezo wa sikio kujisafisha……ndiyo, sikio linaweza kujisafisha.
Katika usafi wa mwili, kila mtu anafahamu namna anavyo usafisha na kuutunza mwili wake, je unapoamka asubuhi ni jambo gani unakumbuka la kwanza linalo husiana na usafi wa mwili wako?, na je ni mara ngapi umewahi kuamka na kufikiria juu ya usafi wa masikio?.
Sehemu ya nje ya sikio (Outer Ear) ndiyo inayohusika au kuhusishwa na usafi, sehemu hii pia hufanya kazi ya kukusanya mawimbi ya sauti na kuyaongoza kufika sehemu ya kati ya sikio. Katika sikio huwa kinatengenezeka kimiminika chenye asili ya mafuta na mchanganyiko wa seli za mwili zilizokufa pamoja na nywele, jina la kimiminika hiki ni nta (Earwax or Cerumen). Kwa kawaida tunapofanya usafi wa masikio huwa tunasafisha ili kuondoa nta, vumbi pamoja na uchafu mwingine.
Katika hali ya kawaida na kwa jinsi sikio lilivyoumbwa, linao uwezo wa kujisafisha kwa maana ya kwamba, nta inayotengenezeka sikioni hutolewa na sikio. Hii hufanyika kwa sehemu za ndani/kati za sikio ambazo siku zote huwa zinasogea (Movement) na kusukuma nta itoke ndani ya sikio ije nje na pia kwa namna ambavyo taya (jaws) zinafanya kazi, husaidia kusukuma nta itoke nje ya sikio.
Pamoja na sikio kuwa na uwezo wa kujisafisha (kutoa nta nje), kuna mazingira ambayo mtu utalazimika kulisafisha sikio, mfano umeugua sikio au umechafuka masikio kwa vumbi au uchafu mwingine, hapo utahitaji kuyasafisha.
Mara nyingi tunatumia pamba maalumu kuyasafisha masikio (Cotton Swab), katika utumiaji wa pamba hizi ni vyema tukawa makini kwani, kwa kuzisukuma pamba ndani sikioni, pia tunaisukuma nta iingie ndani zaidi, hii huweza kupelekea nta ikaziba ngoma ya sikio (Eardrum) na kupelekea mtu kupoteza uwezo wake wa kusikia, pia pamba inaweza kukwama sikioni ikakusababishia matatizo (Ear Infection).
Kama unayo matatizo ya masikio mfano masikio kujaa nta, unaweza kutumia kitambaa safi kuyasafisha au dawa za kuondoa nta (Hydrogen Peroxide) au ukaonana na wataalamu wa afya ili kupata msaada zaidi.
Miongoni mwa kazi zinazofanywa na nta katika sikio ni, kulilinda sikio dhidi ya magonjwa (Antibacterial), kulainisha sikio, kunasa vumbivumbi lisiingie sikioni, na pia kurekebisha mawimbi ya sauti yaingiayo sikioni.
Tuwe makini tunapokuwa tunayasafisha masikio yetu ingawaje kuna namna yanaweza kujisafisha.
Chanzo: Tanzlife Company Limited
2 Comments