Imeelezwa kuwa tatizo la afya ya akili kwa wazee huenda likaongezeka nchini kutokana na takwimu zilizotolewa hivi karibuni na ofisi ya taifa ya takwimu kuonyesha kuwa Tanzania ina wazee milioni 2.5.
Kulingana na takwimu hizo mkoa wa Kilimanjaro ndio unaongoza kwa kuwa na wazee wengi ambao ni asilimia saba ya wazee wote nchini.
Takwimu ulimwenguni zinaonyesha kuwa watu wenye umri wa miaka 60 na kuendelea ni zaidi ya milioni 800 duniani na kwamba makisio yanaonyesha kwamba idadi hiyo itaongezeka hadi kufikia zaidi ya bilioni moja ifikapo mwaka 2050.
Akizungumza kuhusu siku ya Afya ya Akili Duniani, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi, alisema taarifa ya magonjwa ya akili ya mwaka 2012/13 inaonyesha kuwa takribani wazee 13,789 walihudhuria kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya nchini.
“Idadi hii ndogo ya mahudhurio inachangiwa na uelewa mdogo wa jamii kuhusiana na matatizo mbalimbali ya afya ya akili kwa wazee,”alisema Dk Mwinyi.
Hata hivyo alisema matatizo ya afya ya akili kwa wazee hayatambuliki kwa urahisi na jamii na hata kwa watoa huduma wa afya.
Kwa mujibu wa waziri huyo magonjwa yanayoathiri wazee kwa wingi ni pamoja na Sonona/huzuni (Depression), Udhahifu wa fahamu (Dementia), Kisukari, Saratani za aina mbalimbali na Shinikizo kubwa la damu na magonjwa ya moyo.
Pia alisema ziko sababu mbalimbali ambazo hupelekea wazee kupoteza uwezo wa kuishi kwa kujitegemea kama vile kupoteza uwezo wa kutembea, kupungua kwa uwezo wa kuona na udhahifu wa kimwili kutokana na uzee au matatizo mengine ya kiakili ambayo hupelekea kuhitaji huduma za kiafya na kijamii kwa muda mrefu.
Waziri huyo alisema viko visababishi vingi ambavyo husababisha matatizo ya afya ya akili kwa wazee yakiwemo umaskini, kutengwa na jamii, kuwa tegemezi, upweke na upotevu wa vitu mbalimbali mfano kufiwa na mtu wa karibu, kupoteza mali, kupoteza kazi au kuwa mlemavu, kukosa huduma muhimu, unyanyapaa, unyanyasaji na ubaguzi.
“Magonjwa ya mara kwa mara na ya muda mrefu ni hali ya kawaida kwa wazee walio wengi hali hii inahitaji uangalizi na matunzo maalum ya kitaalam,”alisema.
Pia alisema utaratibu wa kutoa huduma bure kwa wazee bado una mapungufu kwani wazee walio wengi hasa wa vijijini wanaachwa nje ya utaratibu wa kupata huduma kutokana na kushindwa kuthibitisha kwamba wana umri wa miaka 60 na hawana uwezo wa kuchangia gharama hizo.
Kaulimbiu ya siku ya afya ya akili duniani mwaka 2013 ni ‘Afya ya Akili kwa Wazee’ ambayo inalenga kuhamasisha jamii juu ya matatizo mbalimbali ya afya ya akili yanayowakabili wazee katika jamii.
Chanzo: Tanzlife Company Limited