Articles

MATATIZO YA ULAJI WA CHAKULA (EATING DISORDERS)

By

on

MATATIZO YA ULAJI WA CHAKULA

MATATIZO YA ULAJI WA CHAKULA

 

Matatizo ya ulaji wa chakula (Eating Disorders) ni namna ambayo siyo ya kawaida ya ulaji wa chakula ambapo mtu anaihatarisha afya yake au maisha yake aidha,  kwa kula chakula kingi sana au kidogo sana ukilinganisha na hitaji halisi kwa ajili ya afya yake ya mwili au akili.

Mwili wa binadamu ili uweze kuwa katika afya nzuri kwa maana ya mwili kuwa na nguvu pamoja na uwezo wa kujilinda dhidi ya magonjwa mbalimbali, unahitaji chakula.

Katika maisha ya kila siku, mwili wako jinsi ulivyo inategemeana na wewe unaulisha kitu gani. Matatizo ya kula chakula yamegawanyika katika makundi yafuatayo:

Kundi la kwanza hujumuisha watu ambao wanaamini kuwa wao ni wanene sana  ingawaje kwa hali halisi ni wembamba kiasi cha kutisha na wanajinyima kula chakula mpaka kufikia hatua ya kuhatarisha maisha yao. Kundi hili kwa kitaalamu huitwa, Anorexia nervosa.

Kundi la pili hujumuisha watu ambao hula chakula kingi kuliko uwezo wa tumbo na baadaye ili waweze kuwa katika hali nzuri huamua kujisafisha tumboni aidha kwa kujitapisha au kwa kutumia dawa za kuwawezesha kukipunguza kwa njia ya haja kubwa (Laxatives).Kundi hili kwa kitaalamu huitwa, Bulimia nervosa.

Kundi la tatu hujumuisha watu ambao wao hawana utaratibu maalumu unaoeleweka wa kula chakula na hawawezi kujitawala katika ulaji wa chakula, kwa kitaalamu kundi hili huitwa, Binge eating.

Msingi wa tatizo la ulaji wa chakula ni mgumu, ila miongoni mwa mambo ambayo hupelekea watu kuwa na matatizo haya ni kama vile: Mtu kuwa na mawazo (Depression), kutaka kuwa na umbo Fulani la mwili ili uweze kufanya kazi ya aina Fulani mfano wanamichezo, ma-model au ma-miss, mtu kufokewa kwa uzito wa mwili wake, umbo lake au namna anavyokula chakula, kuwa katika hali ngumu mfano katika kazi au kimasomo na pia tafiti zinaonyesha kuwa tatizo hili la kula chakula linahusiana na kurithi katika familia.

Ili tuweze kujitambua namna tunavyokula chakula na kuchukua hatua zinazostahili, ni vyema tukazifahamu dalili za matatizo haya ya ulaji wa chakula. Miongoni mwa dalili hizo ni kama vile: Mtu kulaumu kuwa ana uzito mkubwa ingawaje uzito wake upo sawa au ni mdogo kuliko unavyostahili, mtu huandaa chakula kingi au chenye matayarisha magumu lakini atakula kidogo sana na kukiacha, mtu kutokula chakula muda unapofika wa kula.

Matatizo ya kula chakula husababisha madhara mbalimbali kiafya na hata kijamii. Kiafya hupelekea mtu kudhoofika mwili, kupata vidonda vya tumbo, matatizo ya akili na madhara mengine, kijamii husababisha migogoro katika familia, maeneo ya kazi na kuathiri uwezo wa mtu kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii.

Je, unatatizo katika namna unavyokula chakula?. Ni vyema tukajitambua na kuchukua hatua sahihi ikiwa ni pamoja na kuonana na wataalamu wa afya ili kuweza kupata msaada zaidi wa kitaalamu na kupunguza au kuondoa madhara yanayotokana na matatizo ya ulaji wa chakula (Eating Disorders).

Chanzo: Tanzlife Company Limited

About Admin

Avatar

Recommended for you

1 Comment