Sayansi na Tekinolojia ni kitu muhimu katika maisha yetu ya kila siku. Utendaji wa mambo mengi umekuwa rahisi zaidi na pia ubora wa vitu umebadilika kupitia sayansi na tekinolojia.
Jambo la kukumbuka ni kwamba, kila kitu kina uzuri na ubaya wake, hivyo hivyo, sayansi na tekinolojia ina uzuri na ubaya wake.
Katika mambo ya afya ya binadamu na viumbe hai wote kwa ujumla, sayansi na tekinolojia imeleta mapinduzi makubwa sana ikiwa ni pamoja na kuwezesha tafiti za magonjwa kufanyika kwa urahisi na pia kuboresha utoaji wa tiba za magonjwa mbalimbali.
Kwa kuwa ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku, siyo vibaya tukakumbushana kuwa sayansi na tekinolojia pia inazo hasara zake ambazo kwa namna moja au nyingine hasara hizo hugharimu afya zetu au maisha yetu kama watu tunaoenda sambamba na sayansi na tekinolojia.
Kama mtu wa ngazi ya kawaida, ambayo ndiyo watu wengi tupo, utakubaliana na mimi kuwa vitu vingi tunavyovitumia katika maisha yetu ya kila siku ni vile ambavyo tumeviandaa au ambavyo vimeandaliwa kwa kutumia tekinolojia ambayo siyo kubwa, na ndiyo maana tunaweza kumudu gharama, pia vipo baadhi ya vitu tunavyo vitumia ambavyo vimeandaliwa kwa tekinolojia ambayo siyo ndogo lakini mtu wa kawaida unaweza kukipata kitu hicho na kukitumia.
Baadhi ya maeneo ambayo sayansi na tekinolojia inagusa afya zetu moja kwa moja ni kama vile: Dawa, chakula, vinywaji, kazi (mfano kiwandani), vitu vya urembo na vipodozi na vingine vingi.
Tekinolojia ndogo inapotumika kuandaa kitu, maana yake ni kwamba hata ubora wa kitu hicho pia siyo mkubwa, kama ni kitu kinachotumika moja kwa moja katika mwili wa binadamu, mfano chakula, dawa au kipodozi, vitu hivyo vinakuwa na uwezekano wa kuwa na mabaki au vitu vingi ambavyo havihitajiki mwilini kwani tekinolojia ndogo iliyotumika kuandaa vitu hivyo haikuweza kuvisafisha zaidi na hivyo kuleta uwezekano wa mtumiaji kupata madhara bila yeye kufahamu.
Sehemu nyingine katika tekinolojia ni sisi wenyewe kutumia vitu tofauti na inavyopaswa, mfano utumiaji wa dawa za binadamu katika kuwalisha au kutibu mifugo. Yawezekana kwa kufanya hivyo ukaona faida au matokeo mazuri kwa mifugo yako, lakini swali la msingi ni hili, unapomlisha kuku au nguruwe dawa za binadamu kutakuwa na madhara gani kwa mtumiaji wa zao au mlaji wa hao kuku au nguruwe?. Moja ya tatizo kubwa linaloletwa na utumiaji wa dawa za binadamu kwa mifugo ni, kujenga usugu wa vijimelea vinavyosababisha magonjwa (Antimicrobial Resistance), ambapo dawa nyingi zinapoteza uwezo wake wa kutibu magonjwa mbalimbali kwa wanadamu.
Ni kweli kwamba sayansi na tekinolojia ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku, lakini tuwe waangalifu zaidi katika kuitumia ili tuweze kuwa na afya imara na kuboresha maisha yetu.
Chanzo: Tanzlife Company Limited