Ngiri au Hernia ni aina ya ugonjwa ambao unampata mtu baada ya misuli au kuta za tishu mwilini zinazoshikiria au kubeba viungo (organs) fulani mwilini kupoteza uimara wake au kuwa na uwazi (Opening) na hivyo kusababisha viungo hivyo kutoshikiriwa ipasavyo katika sehemu vinapostahili kuwepo.
Katika mwili wa binadamu, maeneo ambayo tatizo hili hutokea mara kwa mara ni maeneo ya tumboni, katika eneo la kinena, eneo la paja kwa juu na pia ngiri inaweza kutokea katika eneo ambalo mtu alifanyiwa upasuaji (operesheni).
Tatizo la ngiri huweza kumpata mtu yeyote. Miongoni mwa vitu vinavyoweza kumsababisha mtu apate ugonjwa wa ngiri ni: Kuwa na uzito mkubwa wa mwili au kuongezeka uzito kwa ghafla, kazi ya kubeba au kunyanyua vitu vizito, tatizo la kukohoa au kupiga chafya kwa muda mrefu, ujauzito au matatizo yanayojitokeza kwa mwanamke wakati wa kujifungua pia kuharisha au kuvimbiwa (Constipation). Vitu hivyo pamoja na mtu kuwa na misuli au tishu zilizopoteza uimara au uwazi (opening or hole) humfanya mtu apate ngiri (hernia).
Ngiri hutambuliwa kwa kutokea kitu kama uvimbe au kujaa katika eneo husika (baadhi ya maeneo yametajwa hapo juu) na pia kwa kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara na daktari huwezesha kugundua tatizo hili.
Njia inayoweza kutatua tatizo hili ni kwa mtu mwenye ngiri kufanyiwa upasuaji ili kurekebisha misuli au tishu zilizolegea. Pia kutegemeana na kihatarishi cha tatizo hili, mtu unaweza kuwa unafanya mazoezi ili kupunguza uzito wako na kuweka utaratibu mzuri wa kula chakula kinachojumuisha mboga mboga au matunda yenye nyuzi nyuzi (fibers), hii itasaidia pia mmeng’enyo (digestion) wa chakula tumboni na kuepusha kuvimbiwa. Matunda (Vitamin C) husaidia kuunganisha tishu zilizolegea na pia husaidia kupona haraka kwa sehemu iliyofanyiwa upasuaji (operesheni). Na kama tatizo lako ni la kukohoa kwa muda mrefu kunakosababishwa na uvutaji wa sigara, ni vyema ukasitisha uvutaji ili kupunguza madhara au makali ya ngiri lakini pia kusitisha sigara kwa ajili ya usalama wa afya yako.
Chanzo: Tanzlife Company Limited
80 Comments