Articles

KUWA NA MALARIA ZAIDI YA 4

By

on

MBU ANAYEENEZA MALARIA

MBU ANAYEENEZA MALARIA

Malaria ni ugonjwa hatari unaoenezwa kwa njia ya kung’atwa na mbu waliobeba vijidudu vinavyosababisha malaria, Plasmodium malariae.

Pamoja na kuwepo jitihada mbalimbali za kupambana na ugonjwa huu, bado unasababisha vifo vingi vya watu na hasa watoto wadogo wenye umri wa chini ya miaka mitano na pia vifo vya wamama wajawazito.

Mpenzi msomaji na mfuatiliaji wa taarifa mbalimbali za mambo ya afya kupitia Blog yako ya Tanzlife, utakubaliana na mimi kuwa, inakuwa ni jambo la ajabu sana kwa baadhi ya watu wakisikia kuwa mtu ana malaria zaidi ya nne (4), au inakuwa ni vigumu mtu kuelewa kwa ufasaha kuwa hata hiyo malaria 3 , 4 au idadi yoyote ile aliyokutwa nayo inamaanisha kitu gani.

Katika mada hii napenda kukushirikisha juu ya maana ya idadi ambayo mgonjwa anaandikiwa katika cheti chake mara baada ya kufanyiwa vipimo vya maabara kuhusu ugonjwa wa malaria.

Kwanza kabisa tuanze na ufafanuzi kwa ufupi kuhusu vijidudu vinavyosababisha malaria, vijidudu hivi ambavyo husababisha malaria kwa ujumla hujulikana kama Plasmodium malariae ingawaje kuna makundi tofauti tofauti ambayo husababisha ugonjwa huu likiwemo kundi la wadudu wajulikanao kama Plasmodium falciparum. Vijidudu hivi huenezwa kwa njia ya kung’atwa na mbu aliyevibeba, na baada ya kukung’ata husababisha viingie katika mfumo wako wa damu na kupelekwa mpaka kwenye ini ambapo vijidudu hizi vitakuwa vinazaliana, baada ya muda fulani vinakuwa vinatolewa na kurudi kwenye damu na ndipo utaanza kuhisi homa na vipimo vya damu vikifanyika vijidudu hivi vinaweza kuonekana.

Katika damu ya mwanadamu kuna vitu vingi, katika mada hii tutagusia tu kuhusu chembe hai za damu ambazo katika vipimo ndizo hasa zinahusika, chembe hai nyeupe za damu (White Blood Cells, WBC), kwa wastani mtu anazo chembe hai hizi kiwango cha elfu sabini katika damu yake. Kipimo cha malaria hufanyika kwa kuchukua kiasi kidogo tu cha damu na kukiangalia kupitia darubini baada ya kukichangana na rangi maalumu (pigment), na katika kufanya uchunguzi, uwezo wa darubini nyingi zinaangalia wadudu wa malaria katika chembe hai mia mbili, hii ni kutokana na uwezo wa darubini (Eyepiece). Na ndiyo maana katika majibu unayoandikiwa huwa unaandikiwa kuwa una vijidudu mfano vitatu, itaandikwa 3/200 WBC, tafsiri yake ni kwamba, unavyo vijidudu vitatu vya malaria katika chembe hai mia mbili zilizowekewa hiyo rangi maalumu na kuchunguzwa kwa msaada wa darubini, lakini mwilini mwako haina maana kuwa unazo chembe hai mia mbili peke yake, bali ni zaidi ya hapo, karibu elfu sabini, hivyo ukihitaji kujua mwilini mwako una wastani wa vijidudu vingapi vya malaria utafanya mahesabu ya kawaida tu, chukua uwiano wa vijidudu vitatu katika chembe hai mia mbili, na angalia je katika mwili mzima wenye chembe hai zaidi ya elfu sabini utakuwa na vijidudu vingapi, utapata jibu.

Pia kwa watu ambao wakifanyiwa vipimo wanasema hawana malaria, ukweli ni kwamba inawezekana kweli ukawa hauna malaria, ila kwa upande mwingine inawezekana ukawa unayo ila tu haijaonekana pengine bado vijidudu vipo katika ini vinazaliana.

Mpenzi msomaji, kwa ufafanuzi huo natumai utakuwa umepata kitu fulani kuhusu kipimo na ugonjwa wa malaria, na utaona kwamba swala la mtu kuwa na malaria tatu, nne au zaidi ni kitu kinachowezekana, mfano kwa wale tunaosikia kuwa malaria imepanda kichwani (Cerebral Malaria), utakuta katika chembe hai mia mbili mtu huyu akawa na vijidudu hata zaidi ya kumi, na ukitafuta katika mwili mzima utaweza kupata idadi ambayo kama hujapata ufananuzi wowote unaweza kuhisi ni kitu kisichowezekana kabisa.

Ahsante sana kwa kuwa mfuatiliaji wa habari na dondoo za afya, endelea kupata taarifa hizi kupitia Blog yako ya Tanzlife, na pia kama una maswali au una mada ambayo ungependa kuipatia ufafanuzi au iwekwe katika Blog hii, usisite kutuandikia kupitia ukurasa wetu wa Facebook (Tanzlife), au kupitia barua pepe, info@tanzlife.co.tz, au tanzlife.health@gmail.com.

Afya ni mtaji

Chanzo: Tanzlife Company Limited

About Admin

Avatar

Recommended for you

1 Comment