Nywele ni sehemu katika mwili wa binadamu na hivyo zinatakiwa kupewa uangalizi kama ambavyo sehemu nyingine za mwili zinavyopewa uangalizi.
Miaka ya hivi karibuni, watu wengi wamekumbwa na matatizo ya kuwa na upara na hususani kwa vijana wenye umri wa kuanzia miaka 20 – 25. Watu wana mitazamo tofauti kuhusu upara ( wapo wanaoamini upara ni ishara ya kuwa na elimu sana au kuwa na busara sana), lakini leo napenda kukufahamisha vitu kadhaa ambavyo vinaweza kumfanya mtu apate upara.
Mpenzi msomaji, kitu cha kwanza kinachoweza kumfanya mtu apate upara ni matumizi ya pombe katika umri mdogo. Utakumbuka kuwa bidhaa zenye kilevi haziruhusiwi kuuzwa au kutumiwa na watu wenye umri chini ya miaka 18 kwa sheria za Tanzania. Hii ni kutokana na ukweli kuwa kwa watu wenye umri huu miili yao na mifumo mbalimbali katika mwili haijakomaa vizuri na hivyo endapo kilevi (alcohol) itatumiwa, basi itaathiri ukuaji wa mtu huyu ikiwemo swala la afya ya nywele zake.
Kitu cha pili ni, ulaji wa nyama ambayo ilichakachuliwa kwa kumchoma mnyama mfano ng’ombe sindano ili kumuongeza uzito ( sindano ya Oestrogen).
Mtu kuwa na upungufu wa vitamini D, hii imekuwa chanzo cha mtu kupuputika au kunyonyoka nywele na mwinyowe kufikia hatua ya kupata upara.
Mtu kuugua magonjwa sugu au kuwa na magonjwa yasababishwayo na virusi (Viral infection), hii huudhoofisha mwili na kupelekea nywele zinyonyoke.
Kwa wanawake tatizo la upungufu wa damu, anaemia pamoja na matatizo katika kizazi, Polycystic Ovary Syndrome (PCOS), imekuwa chanzo cha nywele kunyonyoka, wanawake huwa na mabadiliko ya mala kwa mala ya homoni mwilini, na baada ya kujifungua mtoto pia, homoni mwilini huwa haziko imara (stable) vizuri na hivyo hukumbwa na tatizo hili.
Maisha ya kukaa sehemu moja bila ya kujishughulisha na kitu au kazi, Sedentary lifestyle, hii hupelekea mwili kuwa na mafuta au cholesterol nyingi ambazo zinaongeza hatari ya kunyonyoka nywele na kupata upara.
Mpenzi msomaji, kwa wapenzi na wafuatiliaji wa mambo ya mpira, watakumbuka mchezaji wa mpira wa miguu katika timu ya Manchester United, Wayne Rooney, alikuwa na tatizo hili, na njia aliyoitumia ni kufanyiwa upandikizi wa nywele ( Hair Transplanting ) kwa gharama ambazo mtu wa kawaida hawezi kuzimudu.
Tatizo la nywele kunyonyoka linaweza kutatulika, njia mojawapo za kuepuka tatizo hili ni kuepuka matumizi ya kilevi, kula chakula au kunywa vinywaji ambavyo havijachakachuliwa, kujishughulisha au kufanya mazoezi pamoja na kufuata maelekezo kutoka kwa wataalamu wa afya kuhusu namna ya kuitunza afya yako.
Chanzo: Tanzlife Company Limited