Kutokana na aina ya maisha tunayoishi kila siku, mambo ya kutafuta elimu, kutafuta ajira, kutafuta wapenzi waaminifu, hizi zote zimekuwa ni miongoni mwa sababu zinazopelekea wanawake wengi kujikuta wanatafuta ujauzito au watoto huku wakiwa na umri wa zaidi ya miaka thelathini na tano, 35.
Kwa mwanamke kuwa mjamzito akiwa na umri wa miaka zaidi ya 35, kuna athari siyo tu kwa mama huyu mjamzito, bali pia kuna athari zinazoweza kujitokeza kwa mtoto atakayekuja kuzaliwa.
Katika ukuaji na kukomaa kwa mwili wa mwanamke ili aweze kupata ujauzito na baadaye kuja kujifungua salama mtoto mwenye hali nzuri kiafya, inawezeshwa na mabadiliko ya kibaiolojia ndani ya mwili wa mwanamke. Mabadiliko haya huletwa na kemikali asilia ndani ya mwili ambazo huitwa kitaalamu, hormone.
Mwanamke anapokuwa amepevuta, mwili wake huwa na kiwango kikubwa cha hizi homoni ambazo humuwezesha kupata mabadiliko muhimu ya kimwili yanayomtambulisha au kumfanya awe na sifa au tabia halisi za mwanamke.
Mpenzi msomaji, kitaalamu homoni hizi kwa mwanamke, uzalishwaji wake mwilini na namna zinavyofanya kazi huwa zina muda maalumu au kikomo cha kutengenezwa mwilini, au hata kama zitatengenezwa basi hazitakuwa katika kiwango cha kutosha na hivyo kumfanya mwanamke kutoyaona baadhi ya mabadiliko ya kimwili ambayo alikuwa akiyaona pindi alipokuwa kijana na hasa chini ya miaka 35.
Athari zinazoweza kujitokeza kwa mwanamke kupata ujauzito akiwa na umri wa zaidi ya miaka 35 ni pamoja na hizi zifuatazo:
Awali ya yote, huwa ni vigumu au ni mara chache sana mwanamke akapata ujauzito akiwa na umri wa zaidi ya miaka 35, hii ni kutokana na mayai kutozalishwa mwilini mwake. Na kama ikitokea akapata ujauzito, mwanamke atakuwa hatarini kupoteza ujauzito wake kutokana na kupungua kwa uwezo wake wa kustahimili ule ujauzito na hivyo mimba kutoka.
Endapo atastahimili kuwa mjamzito katika umri huo, zaidi ya miaka 35, kuna hatari ya mwanamke kupata maumivu makali zaidi wakati wa kujifungua, na hii inasababishwa na kupungua kwa uwezo wa kumsukuma mtoto, shingo ya kizazi kushindwa kufunguka vizuri na pia mtoto kutotoka vizuri. Kutokana na tatizo hili, mwanamke huweza kujikuta akifanyiwa upasuaji au operesheni ili kuweza kumsaidia ajifungue vizuri.
Kwa upande wa mtoto, athari anazoweza kuzipata ni pamoja na hizi zifuatazo:
Mtoto anakuwa katika hatari ya kuzaliwa huku akiwa na ulemavu, mfano, matatizo ya kushindwa kuongea vizuri (ulimi mzito), matatizo ya akili (mtindio wa ubongo), matatizo ya uti wa mgongo, na pia matatizo katika viungo vingine mwilini kama mikono na miguu, kitaalamu tatizo hili huitwa, Down’s Syndrome. Hii husababishwa na mtoto kukosa vitu muhimu wakati alipokuwa tumboni mwa mama yake, na mama yake hakuwa na vitu hivyo (homoni) kutokana na umri wake kuwa mkubwa zaidi.
Mpenzi msomaji, wewe binafsi ndiye unayefahamu aina ya maisha unayoishi, hivyo tafakari na uchukue hatua zinazostahili.
Chanzo: Tanzlife Company Limited
2 Comments