Kutokana na asili katika uumbaji pamoja na ambavyo sisi wanadamu tumezoea kuona, ni kwamba ni jambo la kawaida kwa mwanamme kuota ndevu.
Lakini endapo ndevu zitaonekana zimeota kwa mwanamke, basi kwa baadhi ya watu wataanza kujiuliza ni kwa nini na pengine wakawa na mitazamo tofauti juu ya mwanamke huyu ambaye ameota ndevu. Baadhi watamuona mwanamke huyu kuwa ni mchafu na asiyejipenda na mitazamo mingine mingine ya tofauti.
Mpenzi msomaji leo napenda kukufahamisha japo kwa uchache, mambo ambayo huweza kumfanya mwanamke aote ndevu, na pengine baada ya kukufahamisha utaweza kupata mtazamo wa tofauti juu ya hali hiyo ya kiafya inayojitokeza kwa mwanamke.
Katika mfumo mzima wa uzazi, ndani ya mwili wa mwanamke, kuna viungo vinavyohusika na utoaji wa mayai ambayo baadae huja kurutubishwa na mbegu za kiume na kupelekea mwanamke kupata ujauzito. Viungo hivi vinavyotoa mayai ambavyo huitwa kitaalamu Ovaries, katika hali ambayo siyo ya kawaida Ovaries hizi huzungukwa na kitu kama ngozi na hivyo kupelekea zishindwe kutoa mayai, tatizo ambalo kitaalamu hujulikana kama, Polycystic Ovarian Syndrome (PCOS). Baada ya mayai hayo kushindwa kutoka, hupelekea mwanamke kushindwa kuona siku zake, hedhi, au kuvurugika kwa tarehe ambazo alikuwa amezoea kupata hedhi.
Pamoja na mwanamke kushindwa kupata hedhi, pia miongoni mwa dalili zinazoambatana na tatizo la kufunikwa kwa Ovaries,PCOS, ni kuongezeka kwa homoni za kiume (Androgens) katika mwili huu wa mwanamke.
Ikiwa ni pamoja na kazi nyingine zinazofanywa na homoni hizi za kiume, androgens, pia homoni hizi huhusika na uotaji au ukuaji wa nywele mwilini, na miongoni mwa sehemu ambazo homini hizi hufanya kazi kiharaka ni kama vile maeneo ya kifuani, kidevu, midomo ya juu (Upper lips) pamoja na kwenye mapaja.
Hivyo tatizo hili, PCOS, kwa kuwa huambatana na kuongezeka kwa homoni za kiume mwilini, basi humsababisha mwanamke aote ndevu au nywele katika maeneo hayo niliyoyataja hapo juu. LAKINI, napenda uelewe kuwa tatizo hili la PCOS humsababisha mwanamke aote ndevu, ila SIYO kila mwanamke aliyeota ndevu analo tatizo la PCOS, inawezekana akawa na ongezeko la homoni za kiume lililosababishwa na mambo mengine kama vile matumizi ya dawa.
Mpenzi msomaji, natumai utakuwa umepata chochote juu ya hali hii ya kiafya kwa wanawake, PCOS pamoja na kuota kwa ndevu au nywele. Hivyo ushauri wangu ni kwamba, kwa mwanamke mwenye tatizo hili la kuota ndevu, kwanza aonane na daktari wake au wataalamu wa afya ili waweze kugundua chanzo cha tatizo hilo ili waweze kuandaa mfumo mzuri wa kumsaidia, na pia kama wanajamii tusiwatenge na kuwaona wanawake hawa kuwa ni wa ajabu katika jamii, bali tuwape ushirikiano na kuwapa msaada unaostahili ili waweze kutatua tatizo au hali hiyo ya kiafya kwao.
Chanzo: Tanzlife Company Limited