Articles

KIJUE KIDOLE TUMBO (APPENDIX), MAANA, KAZI ZAKE NA JINSI MTU ANAVYOWEZA KUUGUA APPENDIX

By

on

KIDOLE TUMBO (APPENDIX)

KIDOLE TUMBO (APPENDIX)

Mfumo wa chakula katika mwili wa binadamu huanzia katika kinywa na kumalizikia katika puru ( njia ya haja kubwa). Mfumo huu pamoja na kuhusisha viungo mbalimbali kama vile kongosho na ini, bado muundo wake upo katika namna lilivyo kama bomba, mwanadamu anavyokula pamoja na kunywa vinywaji, vyote hivyo vikishaingia mwilini kuna njia ambayo tena taka-mwili hutolewa nje ya mwili. Muundo huu mfano wa bomba kwa urahisi ndiyo tunaouita utumbo katika mwili.

Katika mwili wa binadamu, utumbo umegawanyika katika sehemu tofauti tofauti, na sehemu moja wapo ambayo kutokana na mada hii tutaigusia ni sehemu ya utumbo mpana ambao kwa kitaalamu huitwa colon au large intestine. Sehemu hii ya utumbo mpana katika mwili wa binadamu yenyewe moja ya kazi zinazoifanya katika mwili ni kufyonza au kunyonya maji kutoka katika mabaki ya vyakula vilivyovunywavunjwa na mwili kwa njia ya mmeng’enyo au kwa kitaalamu, Digestion.

Utumbo mpana, unayo sehemu iliyojitokeza yenye sura au umbo la kidole  ambayo kwa kitaalamu huitwa Appendix, na sisi kutokana na jinsi umbo lake lilivyofanana na kidole, tumezoea kuiita sehemu hii, kidole tumbo. Katika mwili, sehemu hii ipo upande wa kulia chini ya tumbo.

Mpenzi msomaji, kidole tumbo katika mwili wa binadamu husaidia vitu mbalimbali, mfano, katika mmeng’enyo wa chakula. Mwili wa binadamu pamoja na vitu vingine vyote vinavyoufanya ufanye kazi zake vizuri, pia mwili huu unao viumbe wengine wasiokuwa waharibifu wanaoufanya mwili ufanye kazi zake kwa uzuri zaidi. Viumbe hawa wasiokuwa waharibifu ni bakteria ambao kwa kitaalamu huitwa normal flora. Bakteria hawa hupatikana katika kinywa, ngozi, tumboni na hata katika sehemu hii ya utumbo mpana tunayoiita kidole tumbo au appendix.

Baadhi ya bakteria wasiokuwa waharibifu wanaopatikana katika kidole tumbo husaidia katika uvunjwaji au ulainishaji wa vyakula vya nyuzi nyuzi (fibres)  ambavyo tunakula kila siku. Pamoja na kusaidia katika mmeng’enyo wa chakula pia tafiti za kisayansi huonyesha kuwa, appendix husaidia katika uzalishaji wa kinga za mwili, antibodies (immunoglobulin A) ambazo husaidia kupambana na kuua wadudu waharibifu ambao huingia katika matumbo yetu kupitia chakula.

Katika huduma za upasuaji zinazotolewa, appendix pia imekuwa kama sehemu ya kiungo mbadala ambacho mtu huweza kufanyiwa upasuaji, appendix ikatolewa na ikaunganishwa sehemu nyingine katika tumbo au mfano mfumo unaohusu utoaji mkojo mwilini na appendix hii ikawa ni kiunganishi katika sehemu ya mirija fulani yenye shida tumboni (Reconstructive surgery).

Asilimia kubwa ya ugonjwa wa kidole tumbo, husababishwa na bakteria waharibifu ambao kupitia njia mbalimbali mfano kula chakula, au mwili kuwa na maambukizi ya magonjwa ( infection) huweza kusababisha kidole tumbo kivimbe au kiathirike na kumfanya mtu aanze kupata matatizo ya kiafya.

Baada ya kidole tumbo kuathirika, miongoni mwa dalili ambazo mtu huanza kupata ni pamoja na: Maumivu sehemu ya chini ya tumbo upande wa kulia ambapo maumivu haya huweza kusambaa mpaka mguu wa kulia, kuhisi kichefu chefu na kutapita,kukosa hamu ya kula chakula,  kupata maumivu makali chini ya tumbo upande wa kulia pindi unapovuta pumzi kwa nguvu, kupatwa na homa, kuharisha na endapo hatua stahiki hazitochukuliwa, basi kidole tumbo huweza kupasuka na kupelekea mchafuko wa damu na matatizo mengine ndani ya mwili.

Tatizo au ugonjwa unaoathiri kidole tumbo, kitaalamu, appendicitis, huweza kugundulika mapema na kutatuliwa kabla ya kuleta madhara makubwa kwa mtu, hivyo ni vyema ukapata ushauri wa wataalamu pindi uonapo au unapohisi kuwa na dalili hizo hapo juu kuhusu hali yako ya kiafya

Chanzo: Tanzlife Company Limited

 

 

About Admin

Avatar

Recommended for you

17 Comments