Malaria ni ugonjwa unaosababishwa na vijidudu ambavyo kitaalam hujulikana kwa jina la plasmodium, jamii hii ya wadudu imegawanyika katika makundi tofauti tofauti na kundi ambalo hasa hasa husababisha ugonjwa huu hatari ni kundi lijulikanalo kwa jina la Plasmodium malariae.
Ugonjwa huu wa malaria huenezwa na mbu jike ( kitaalamu huitwa Anopheles) ambaye amevibeba vijidudu visababishavyo malaria kutoka kwa mtu mwenye malaria. Pindi mbu huyu anapomng’ata mtu, humuachia vijidudu visababishavyo malaria na hapa ndipo vijidudu huanza kuzaliana ndani ya mwili wa binadamu na kumfanya aanze kupata madhara ya kiafya kama vile homa, maumivu ya viungo na hasa hasa maumivu ya jointi, maumivu ya kichwa, kukosa hamu ya kula chakula, na endapo hatopata matibabu mapema huweza kuishiwa damu na hata kupoteza maisha.
Mpenzi msomaji, mtu yeyote huweza kuugua ugonjwa huu wa malaria, ila kuna tofauti kadhaa katika miili yetu kama wanadamu zinazofanya baadhi ya watu waugue mara kwa mara na wengine huchukua muda mrefu kusikia kaugua, mbali na kuugua malaria pia inawezekana tofauti hizi zikawepo katika uuguaji wa magonjwa mengine. Moja ya sababu zinazopelekea utofauti huu ni kutofautiana uwezo wa kinga ya mwili, kuna baadhi ya watu wana kinga ya mwili imara, na kinga imara ya mwili hujengwa na lishe nzuri. Ulaji wa matunda na mboga za majani husaidia kujenga kinga imara ya mwili na hivyo mwili hupata uwezo mkubwa wa kupambana na magonjwa.
Pamoja na kwamba kibinadamu miili yetu imetofautiana, kwa upande wa mwanamke mjamzito swala hili liko tofauti kidogo, mwanamke pindi anaposhika ujauzito tayari ndani ya mwili wake kuna mifumo mingi ambayo inabadilika kiutendaji kazi ili kuendana na hali ya ujauzito aliyonayo na hii unaweza kusema kuwa ujauzito humfanya mwanamke awe mtu mwingine tofauti na alivyokuwa mwanzo, hii ni kutokana na kubadilika kwa vitu vingi siyo tu ndani ya mwili wake, lakini pia hata kwa nje waweza kuona mabadiliko haya mfano tabia, anaweza kuanza kukichukia au kukipenda kitu, ulaji hubadilika, huanza kubagua vyakula tofauti na wakati hajawa mjamzito, haya ni baadhi tu ya mabadiliko unayoweza kuyaona kwa nje.
Mwanamke mjamzito ndani ya mwili kila kinachoingia kinagawanywa, kwa ajili yake na pia kwa ajili ya ujauzito (mtoto au watoto). Hii ni katika vyakula anavyokula mama mjamzito, vinywaji na chochote kile kinachoweza kuingia ndani ya mfumo wa mwili ikiwemo dawa. Kutokana na mahitaji ya mwili kuwa makubwa kwa mama mjamzito hii humfanya kinga yake ya mwili iwe chini ukilinganisha na mwanamke asiyekuwa mjamzito, sababu hii humfanya awe hatarini zaidi kuugua magonjwa na hasa ugonjwa huu wa malaria ambao kwa kiasi kikubwa umekuwa chanzo cha vifo kwa wajawazito wa watoto.
Ili kuweza kusaidia kundi hili dhidi ya ugonjwa huu hatari, inashauriwa wajawazito walale katika chandarua chenye dawa ya kuuwa mbu wasambazao vijidudu vya malaria na pia watumie dozi ya malaria mara mbili katika kipindi chote cha ujauzito yaani katikati ya juma la 20 – 24 na juma la 28 – 32 na aina ya dawa wanayopaswa kutumia ni SP ( Sulphadoxine Pyrimethamine), hii husaidia kupunguza athari za malaria pindi ikitokea mama mjamzito akapatwa na malaria.
Mpenzi msomaji, japo kwa uchache natumai utakuwa umepata na kuielewa mada hii. Endelea kufuatilia dondoo mbalimbali zinazohusu afya kwa ujumla ili uweze kuyafahamu zaidi mambo muhimu ya kufanya katika tiba ya ugonjwa fulani, namna ya kuepukana na magonjwa na hata kujilinda kiafya. Haya yote hupatikana katika blog yako ya Tanzlife.
Chanzo: Tanzlife Company Limited
Pingback: ZIJUE SABABU ZA WAJAWAZITO KUWA HATARINI ZAIDI KUUGUA MALARIA KULIKO WATU WENGINE | Blog Mama