Articles

HALI YA UTEJA ( DRUG ADDICTION )

By

on

DAWA ZA KULEVYA

DAWA ZA KULEVYA

Uteja ( Drug Addiction ) ni hali anayokuwa nayo mtu baada ya kuwa ameanza utumiaji wa dawa ambazo zinasifa ya kumfanya mtumiaji ashindwe kujitawala katika kuzitumia, na pindi akiacha kuzitumia anapata dalili mbaya kimwili au kiakili na hivyo kumfanya azitafute dawa hizo ili atumie na kumfanya ajihisi vizuri. Jina ambalo limezoeleka kwa watu wengi la dawa hizi ni, dawa za kulevya.

Yapo mambo mbalimbali yanayomfanya mtu aanze kutumia dawa za kulevya na hatimaye kuwa mteja (teja), miongoni mwa mambo hayo ni kama vile:

Mtu kuwa na marafiki wanaotumia dawa hizo na hivyo ili kuendeleza urafiki mtu anajikuta anaanza kutumia ili asiwaangushe marafiki zake (mob psychology).

Msongo wa mawazo, mtu anaona akitumia dawa hizi itamsaidia kuondoa mawazo yaliyomjaa kichwani ambayo hayampatii furaha yoyote katika maisha yake.

Mtu kutaka kujaribu/kutumia kila kitu, hii inatokea kwamba mtu hana sababu zozote zile ila tu anataka ajaribu kutumia dawa hizo ili aone nini kitatokea na mwisho wake anakuwa teja.

Jambo ambalo yawezekana ungependa kufahamu ni kwamba, kwa nini dawa hizi husababisha mtu awe mteja/teja wakati kuna dawa zipo nyingi ambazo hazisababishi tatizo hili la uteja?. Utendaji kazi wa dawa hizi mwilini tunazoziita dawa za kulevya ni mgumu, ila kuna sifa hizi mbili ambazo zinaweza kulielezea jambo hili, sifa ya kwanza inahusika na mwili wa binadamu hususani sehemu kuu ambapo dawa hizi za kulevya huhusika sana, katika mfumo wa fahamu (ubongo), ubongo wa binadamu umeumbwa kwa chembe hai (Cells) ambazo ni laini sana (Very Delicate) ukilinganisha na seli za sehemu nyingine ya mwili, hivyo ni rahisi sana kubadilika kutegemeana na mazingira unayouzoesha ubongo wako, jinsi utakavyo uzoesha ndivyo utakavyokuwa. Pili ni sifa ya dawa zenyewe za kulevya, ambapo zinasifa ya kubadilisha utendaji kazi wa chembe hai (Cells) katika mfumo wa fahamu na kuzifanya zifanye kazi kuendana na dawa yenyewe husika, hivyo ubongo wako hautojitawala bali kazi za ubongo zitatawaliwa na dawa, na kwa kuwa seli za ubongo ni rahisi kubadilika, itapelekea kwamba utendaji kazi wake utazoea (adaptation) kufanya kazi kwa msaada wa dawa na hivyo ukiacha kutumia unajikuta mwili/ubongo hauko tayari kufanya kazi bila dawa na hatimaye utaanza kuitafuta ili ubongo uweze kurudi katika hali ambayo uliuzoesha ya kutumia dawa na hii ndiyo huitwa sasa Uteja/teja.

Uteja unayo madhara kwa teja mwenyewe na hata kwa jamii na taifa kwa ujumla, mtu unapokuwa teja unaudhalilisha utu wako, unashindwa kushiriki kikamilifu katika mambo ya kijamii/kazi, unakuwa katika hatari (risk) ya kupata magonjwa mbalimbali kutokana na kuchangia vitu vyenye ncha kali (sindano, viwembe) na pia uteja huchangia familia nyingi ziwe na migogoro.

Kila mwanajamii analo jukumu la kumuelimisha mwenzake juu ya athari zinazotokana na utumiaji wa dawa zinazopelekea mtu kuwa teja (dawa za kulevya), na kwa wale ambao kwa bahati mbaya wamepata tatizo hili, uwezekano wa kupona tatizo hili upo, jambo la kufanya ni kuonana na wataalamu wa afya ili kupata msaada unao stahili.

Chanzo: Tanzlife Company Limited

About Admin

Avatar

Recommended for you