Asilimia kubwa ya sampuli za dawa za mitishamba zinazotumiwa na wanawake wajawazito ambazo zilipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali zimebainika kuwa ni sumu.
Uongozi wa hospitali ya Rufaa ya Amana ulipeleka sampuli 105 kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kujiridhisha baada ya idadi kubwa ya wanawake wanaokwenda kujifungua hospitalini hapo kubainika kuwa wanatumia dawa hizo.
Kwa siku hospitali hiyo inalizalisha wanawake kati ya 100 hadi 120 na kati yao wanawake 10 hubainika kutumia dawa za mitishamba kwa lengo la kuharakisha kujifungua.
Muuguzi Mkuu wa hospitali hiyo Agnes Mwanga, alisema samapuli hizo zilipelekwa mwaka 2009 na baada ya majibu kurudi ilibainika kuwa ni sumu na kwamba zisingeweza kuwasaidia kujifungua.
“Jamii bado haijaelimika vya kutosha kuhusu afya ya uzazi ndio maana kina mama wengi wanachelewa kuripoti hospitali badala yake wanapitia kwanza kwa waganga wa kienyeji na kujikuta wengine wakipoteza maisha,”alisema Mwanga.
Pia alisema vifo vinavyotokana na uzazi vimepungua ambapo kwa mwaka jana vilikuwa 18 kati ya wanawake 29,792.
Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo, Dk Asha Mahita, alisema ni kweli wanawake wengi wamekuwa wakitumia dawa hizo na kwamba wanachofanya sasa ni kuwaelimisha wataalamu wa tiba asili na tiba mbadala kwa sababu wanawake wengi wakishaanza kuumwa uchungu hukimbilia huko.
“Waganga wa tiba asili na tiba mbadala wanatakiwa kuzingatia maadili kama sheria inavyoelekeza na kuepuka kufanya vitendo vya hatari au kutoa tiba ambayo inaweza kusababisha madhara kwa afya au uhai wa mtu,”alisema Dk Mahita.
Kulingana na sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala namba 23 ya mwaka 2002 na kanuni zake, huduma zote za tiba asili na tiba mbadala lazima ziwe zimesajiliwa. Hata hivyo Manispaa hiyo ina waganga zaidi ya 200 lakini waliosajiliwa ni wachache.
Kulingana na sheria hiyo mtu yeyote anayetoa huduma hipo bila kusajiliwa anatenda kosa na akitiwa hatiani anaweza kufungwa jela miaka miwili ama kulipa faini ya Sh500,000.
Licha ya adhabu hizo mahakama pia inaweza kutoa amri kwamba dawa zozote za tiba asili au vifaa vilivyopatikana katika miliki ya mtu aliyetiwa hatiani kutaifishwa, kuharibiwa au kutupwa.
Chanzo: Tanzlife Company Limited