Articles

HOMONI ZA MWANAMKE NA AFYA YA KINYWA

By

on

FIZI NA MENO

FIZI NA MENO

Homoni (Hormones) ni kemikali asilia ambazo huzalishwa ndani ya mwili wa binadamu na kusafirishwa kwa njia ya damu na kusambazwa mwilini ili kutawala mifumo mbalimbali ndani ya mwili na kuufanya mwili ufanye kazi vizuri.

Wanawake hupatwa na mabadiliko ya homoni mara kwa mara hususani homoni za kike ambazo hutawala mifumo yote ya jinsia ya kike (Oestrogen and progesterone). Mabadiliko haya huambatana na kutokea kwa mabadiliko ya kiafya katika kinywa cha mwanamke, hii ni kutokana na kubadilika kwa kiwango cha damu kinachofika katika tishu za kwenye fizi (Gum’s tissues) na hivyo kupelekea fizi kushambuliwa kwa urahisi na magonjwa.

Hatua mbalimbali zinazoambatana na mabadiliko ya homoni kwa mwanamke ni kama zifuatazo:

Anapofikia umri wa kupevuka au kubalehe (Puberty), katika umri huu kunakuwa na ongezeko la homoni za kike (oestrogen and progesterone), kuongezeka kwa homoni hizi hupelekea pia kiwango cha damu kinachofika katika fizi kiwe kikubwa, hii husababisha fizi ziwe nyekundu sana, zijae au kuvimba na kuwa rahisi kuchubuka na kutokwa na damu kinywani wakati unapofanya usafi wa kinywa (Kusukutua meno).

Kipindi cha hedhi (Menstrual period), katika kipindi hiki siyo rahisi kuona mabadiliko katika fizi, ila kuna baadhi ya wanawake fizi zao huvimba, huwa nyekundu na dalili hizi huweza kutokea siku mbili au tatu kabla ya kuanza siku zake, na mara anapokuwa katika siku zake dalili hizi hupungua au hupotea.

Wakati wa ujauzito, kuna msemo unaosema kuwa, pata mtoto…..poteza jino, usemi huu inawezekana ukawa na ukweli kutokana na kwamba, kipindi mwanamke akiwa mjamzito kunatokea mabadiliko makubwa katika uwiano wa homoni mwilini mwake, hii humfanya fizi zake kuwa nyekundu, kuvimba na kushambuliwa kirahisi na wadudu au bakteria na kumsababishia magonjwa ya kinywa (pregnancy gingivitis, periodontitis), magonjwa haya yasipopata tiba humfanya mama mjamzito apoteze jino au meno.

Umri wa kumaliza kuzaa (Menopause), katika umri huu mwanamke anakuwa na upungufu wa homoni za kike (oestrogen) ambazo husaidia kuimarisha mifupa, kupungua kwa homoni hizi humfanya mwanamke kinywa chake au fizi kutoshikiria vizuri meno (mifupa), fizi huvimba, zinakuwa rahisi kuchubuka,rahisi kushambuliwa na bakteria, uwezo wa kuhisi ladha mbalimbali hubadilika, pia anakuwa na hisia kali kwa vyakula au vinywajii vya moto au baridi.

Kutumia vidonge vya majira (Oral contraceptives), vidonge vya uzazi wa mpango huwa na mchanganyiko wa homoni ambazo zinapoingia mwilini hurekebisha uwiano wa homoni katika mwili wa mwanamke na hivyo kupunguza hatari ya kupata magonjwa ya kinywa kwa mwanamke.

Kwa mwanamke ni jambo la kawaida kutokea mabadiliko katika uwiano wa homoni mwilini, na mabadiliko haya yanaweza kukufanya upate dalili ambazo siyo nzuri kwa afya yako, kama utaona dalili ambazo huwezi kuzimudu au kuzitatua kwa uwezo ulionao, usisite kuwaona wataalamu wa afya ili wakusaidie na uendelee kuwa katika afya bora.

Chanzo: Tanzlife Company Limited

 

 

About Admin

Avatar

Recommended for you