Katika hali ambayo ni ya mazoea watu wengi tumekuwa tukitamani na kujitahidi kuwa na mwili wenye umbo au uzito fulani. Hii imekuwa ikifanyika kwa kujiwekea mipaka katika ulaji wa vyakula na pia hata kujihusisha na aina mbalimbali za mazoezi.
Mpenzi msomaji, napenda kuchukua nafasi hii kukushirikisha pamoja na kukukumbusha juu ya uzito wa mwili ambao kiafya mtu anapaswa kuwa nao ili kuweza kuepukana na hatari ya kupata matatizo mbalimbali ya kiafya.
Kwa mujibu wa mahesabu ya kiafya au kitaalamu, uzito wa mwili hutegemeana na urefu wa mtu, ambapo kuna kanuni ambayo kitaalamu huwezesha kujua mtu mwenye urefu fulani anapaswa awe na uzito kiasi gani. Kanuni hiyo ambayo hujulikana kama BODY MASS INDEX (BMI) hutupatia uwiano wa uzito wa mwili wa mtu pamoja na urefu wake.
BMI = Uzito wa mwili katika kilogramu (Kg) / Urefu wa mwili katika mita za mraba (M^2).
Kutokana na kanuni hiyo, ukichukua uzito wa mwili wako katika vipimo vya kilogramu, ukagawanya na urefu wa mwili wako katika vipimo wa mita, utapata namba ambayo kitaalamu itakuwezesha kujua kama uzito wa mwili wako upo sawa kwa maana ya kama ni uzito mkubwa au mdogo.
Mchanganuo wa namba unazoweza kuzipata baada ya kugawanya uzito wako kwa urefu wako ni kama ifuatavyo.
Chini ya 18.5 Mtu huyo anao uzito pungufu ( Under weight )
Kuanzia 18.5 – 24.9 ni Uzito wa kawaida ambao kiafya ni salama ( Normal Weight)
Kuanzia 25 – 29.5 ni Uzito mkubwa ( Over weight )
Kuanzia 30 na kuendelea ni Uzito mkubwa zaidi ( Obesity )
Mfano, inatakiwa ukichukua uzito wako, ukagawanya na urefu wa mwili wako, upate namba ambayo ni kati ya 18.5 na 24.9. Kama una kilogramu 70, na urefu wa mita 1.9, basi ukigawanya utapata, 70/( 1.9)^2 = 19.39 Ambayo kiafya ni sawa. Kumbuka kuwa, urefu wako unatakiwa uwe katika vipimo vya mita na kisha uuzidishe ili kupata mita za mraba, mfano kama una mita 1.9, zidisha hivi, 1.9 mara 1.9 = 3.61, halafu chukua uzito wako mfano, 70kg na gawanya kwa 3.61 utapata 19.39.
Kuwa na uzito pungufu kiafya huleta hatari ya mtu kupatwa na magonjwa kirahisi kwani mwili huwa dhaifu na uwezo wa kupambana na changamoto za kiafya zinazokuzunguka huwa mdogo. Kuwa na Uzito mkubwa pia huuweka mwili hatarini kupatwa na magonjwa kama presha, kisukari na kuhisi ganzi mwilini.
Mpenzi msomaji, ni vyema tukaelewa na kukumbushana juu ya jambo hili ili kwamba, pindi tunapohitaji kujiwekea mipaka katika kula vyakula au pindi tunapofanya mazoezi, basi tuwe na picha kichwani kwamba tunahitaji kupunguza au kuongeza uzito ili ufikie kiwango ambacho kinaendana na urefu wa miili yetu na hivyo kujiepusha na hatari zinazotokana na mtu kuwa na uzito mkubwa au mdogo kuliko inavyopaswa.
Chanzo: Tanzlife Company Limited
3 Comments