Articles

KAFEIN NA MATUMIZI YA DAWA ZA PRESHA

By

on

Kafein (caffeine) ni moja ya vitu ambavyo hupatikana kwa asilia kupitia mazao au mimea ambayo sisi kama wanadamu tumekuwa tukitumia kila siku.

Mimea au mazao ambayo kafein hupatikana ni pamoja na kahawa, chai pamoja na kokoa. Mazao yote hayo tumekuwa tukiyatumia kama kinywaji lakini pia kama kiburudisho.

Inapokuwa katika mwili wa binadamu, kafein huufanya moyo uongeze namna ambavyo unasukuma damu na kuisambaza maeneo mbalimbali ya mwili. Kwa kufanya hivyo inamaana kuwa ufanyaji kazi wa moyo utakuwa umeongezeka.

Miongoni mwa mambo ambayo huweza kumfanya mtu ajisikie kuchoka na kuhisi kama hana mood ni pamoja na kupungua kwa kiasi cha damu ambacho kinafika katika maeneo ya viungo vya mwili na hususani maeneo ya ubongo. Utakumbuka kwamba damu inaposafiri mwilili pia inakuwa inasambaza hewa, chakula, kinga ya mwili na vingine vingi. Hivyo damu ikifika kwa uchache, au ikifika pasipo kuwa na vitu hivyo muhimu, basi itapelekea uhisi mapungufu ya namna flani.

Kafein inapoufanya moyo uongeze namna ambavyo unafanya kazi au kusukuma damu, inamaana kuwa mzunguko wa damu katika mwili unaongezeka na hatimaye kukufanya uwe na hali ya kuchangamka kwani kupitia chai, kahawa au kokoa ambayo umeitumia mzunguko wa damu, hewa na sukari katika mwili na ubongo vyote vitakuwa vimeongezeka.

Kuna nyakati baadhi ya watu wamekuwa wakikosa ama kuchelewa kupata usingizi mara baada ya kutumia moja ya vinywaji hivyo, sababu ni kama ambavyo nimefafanua hapo juu. Pia kutokana na kafein kuwa na uwezo wa kukufanya uchangamke, imekuwa ikichanganywa katika baadhi ya vinywaji jamii ya soda lakini pia hata katika uandaaji wa chocolate.

Tumeona kuwa kafein kupitia vinywaji hivi huongeza ufanyajikazi wa moyo, je vinahusiana vipi na matumizi ya dawa za presha hususani kwa watu ambao tayari wana matatizo ya moyo?.

Matatizo ya moyo yapo na namna tofauti tofauti lakini katika makala hii nichukue nafasi kukufahamisha kuhusu matatizo ambayo yanahusiana na presha ya kupanda na kushuka.

Kwa upande wa watu wenye matatizo ya presha ya kushuka, mara nyingi vinywaji hivi vimekuwa ni msaada mkubwa kwao. Kwani vinaongeza nguvu ya moyo katika kusukuma damu na hatimaye kuifanya presha iongezeke. Pia matumizi ya baadhi ya vinyaji jamii ya soda vimekuwa vikisaidia kupandisha presha na kumpatia mtu nafuu pindi anapokuwa katika hali ambayo siyo ya kawaida.

Kutokana na kafein kuweza kuifanya presha ipande, mara kadhaa imekuwa ikisababisha changamoto katika kupima presha na pia kuandika dozi ya dawa pindi mgonjwa anapokuwa ametumia vinywaji vyenye mchanganyiko huo. Kafein huweza kuifanya presha ipande kwa masaa matatu mara baada ya kuitumia, kwa kufanya hivyo na endapo hapatakuwa na taarifa za matumizi hayo basi huweza kupelekea kwa mtu ambaye hana presha ya kupanda aonekane kama ni mwenye tatizo hilo wakati wa kufanyiwa vipimo. Pia huweza kusababisha mgonjwa akaandikiwa dozi kubwa ya dawa za presha tofauti na uhalisia.

Presha ya kupanda hutibika kwa kuusaidia moyo kupunguza namna ambavyo unasukuma damu na kuifanya mishipa ya damu iwe salama zaidi pamoja na viungo vingine vya mwili.

Dawa zinazotumika kutibu presha ya kupanda, kwa namna moja ama nyingine ufanyajikazi wake unakinzana na kafein. Sababu za presha kupanda moja wapo ni moyo kusukuma damu kwa haraka, kafein pia huufanya moyo usukume damu kwa haraka.

Utaona kwamba kwa mtu mwenye tatizo la presha ya kupanda na yupo katika matibabu, endapo atakuwa ni mtumiaji mkubwa wa kafein itasababisha tatizo la moyo kushindwa kutibika katika muda mwafaka. Miongoni mwa dawa ambazo ufanyaji kazi wake unakinzana na kafein ni pamoja na Propranolol na Metoprolol ambazo ufanyaji kazi wake unakuwa hafifu pindi mtumiaji wa dawa hizo atazitumia sambamba na kafein.

Ili kuweza kuulinda moyo wako na pia kuziwezesha dawa za presha ziweze kufanya kazi ipasavyo, ni vyema kuchukua tahadhari katika matumizi ya kafein kwani ni moja ya vitu vinavyoweza kuifanya presha yako ipande.

Kwa baadhi ya watu ambao wamekuwa watumiaji wa mara kwa mara wa vinywaji vyenye kafein, inafika wakati wakikosa kutumia wanapatwa na maudhi madogo madogo mfano kujisikia kichwa kinauma ama kujisikia kama mwili hauko sawa.

Hii hutokea kutokana na moja ya sifa za chembechembe hii, kafein (caffeine), kwa namna moja ama nyingine huufanya mwili kuwa na hali ya kuizoea na kuihitaji, ambapo kwa kitaalamu hujulikana kama caffeine addiction.

Chanzo: Tanzlife Company Limited

About Admin

Avatar

Recommended for you