Kutokwa na jasho ni njia mojawapo ya mwili kutoa taka na pia ni mfumo unaotumiwa na mwili ili kuupooza pale hali ya hewa au joto la mwili linapokuwa lipo juu.
Katika hali ambayo ni ya kawaida, mwili hutoa jasho baada ya mtu kufanya shughuli fulani ya kufanya joto lake lipande na ili kuliweka katika kiwango cha kawaida, mtu atatokwa na jasho, au yawezekana ikawa siyo kufanya kazi, bali kutokana na mtu kuwa na msisimko fulani, basi jasho linaweza kumtoka.
Kuna baadhi ya watu mpenzi msomaji, ambao mbali na sababu hizo hapo juu, huwa wanatokwa na jasho jingi bila ya kujali kama mtu huyo kakaa amepumzika, hana msisimko wowote, hali ya hewa kuwa nzuri bila joto, yaani haijalishi, wao hutokwa na jasho jingi muda wote. Hili ni tatizo kiafya ambalo kwa kitaalamu hujulikana kama, Hyperhidrosis.
Mpenzi msomaji, baadhi ya matatizo ya kiafya yanayoweza kumfanya mtu apate au awe na tatizo hili la kutokwa na jasho jingi muda wote ni haya yafuatayo:
Pamoja na tatizo hili kuwa gumu kitaalamu, mambo ambayo huhusishwa na tatizo hili ni matatizo ya neva zinazohusiana na glandi za jasho katika mwili na kuzifanya glandi zifanye kazi zaidi ya inavyohitajika, pia tatizo hili huhusishwa na kurithi.
Mambo mengine ambayo husababisha tatizo hili ni matumizi ya baadhi ya dawa, mfano dawa za kuondoa msongo wa mawazo, dawa za kutibu matatizo ya kansa, dawa zinazotumika kutibu magonjwa ya uzazi.
Kuna baadhi ya magonjwa ambayo pia humfanya mtu apate tatizo hili, mfano kifua kikuu, Parkinson, matatizo ya glandi (Over active thyroid gland).
Pia kwa watu wazima na hasa wanawake, hukumbwa na tatizo hili pale umri wao wa kuzaa unapokuwa umeisha (Menopause).
Mpenzi msomaji, ni vyema kama unalo tatizo hili ukawaona wataalamu wa afya ili kuweza kupata msaada unaostahili. Neva zinazotawala glandi za jasho hutumia kemikali asilia mwilini inayojulikana kwa jina la Acetylcholine, na kemikali hii pia huhusika katika mifumo mbalimbali mwilini. Kwa bahati mbaya, dawa zinazotibu tatizo hili huzuia utendaji kazi wa kemikali hii asilia na hivyo, baada ya mtu kutumia dawa huweza kupata madhara kama vile mdomo kuwa mkavu sana na matatizo katika kukojoa.
Chanzo: Tanzlife Company Limited
6 Comments