Kukohoa ni njia inayotumiwa na mwili ili kuhakikisha kwamba njia au mfumo wa upumuaji katika mwili wako unakuwa salama, na hii ni kwa kuhakikisha kwamba vitu kama vumbi, bacteria au kitu chochote kile kisichokuwa salama, basi hakipati nafasi ya kukudhuru wewe kupitia njia ya upumuaji.
Pamoja na kikohozi kuwa njia ya mwili kujilinda, bado unapaswa kuchukua hatua za kupata matibabu zaidi endapo tatizo hili litakuwa endelevu hata zaidi ya wiki moja baada ya kutumia njia tofauti tofauti za kujitibu au kutumia dawa rahisi zinazopatikana katika mazingira ya nyumbani (mfano tangawizi au kitunguu saumu).
Mpenzi msomaji, wewe binafsi unafahamu tatizo la kikohozi unalipa uzito gani, ila ningependa kukufahamisha baadhi ya madhara ambayo huweza kumpata mtu endapo atapuuzia tatizo hili:
Kwanza kabisa utakubaliana na mimi kwamba, endapo mtu anakohoa, basi inamuwia vigumu kuyanyoosha maelezo yake au hawezi kuongea katika mtiririko wa maneno ulio mzuri, hii ni kutokana na kujikuta kila baada ya neno moja au hata kabla hajamaliza kusema neno moja tayari kikohozi kinamkatisha usemi.
Kutokana na kukohoa kusababisha presha kubwa kujengeka katika mdomo na koo, hii hupelekea mtu kupata maumivu ya kichwa na hivyo kukupelekea kupata usumbufu zaidi na kuongeza gharama za matibabu kwako.
Kukohoa kwa muda mrefu husababisha matatizo katika kibofu cha mkojo kwani presha kubwa inajengeka katika kibofu cha mkojo na hivyo kuathiri mfumo wa kawaida wa namna kibofu chako cha mkojo kinavyo stahimili kuhifadhi mkojo na kazi zake kwa ujumla.
Kuna mishipa midogo ya damu katika pua na pia katika njia ya kutolea haja kubwa (Anus), ambapo kwa namna mtu anapokohoa kwa muda mrefu, mishipa hii huweza kupasuka na kupelekea damu kutoka au kusababisha tatizo ambalo kitaalamu hujulikana kama, haemorrhage.
Wakati mwingine kikohozi ni dalili ya magonjwa kama vile, Kifua kikuu, magonjwa ya mapafu kama vile kansa, magonjwa ya moyo ( congestive heart failure ) pamoja na magonjwa ya masikio.
Pia kikohozi kingine husababishwa na matumizi ya dawa, mfano dawa za kutibu presha (High blood pressure) mfano dawa ya Captopril ( ACE- Inhibitor ), na hivyo kuhitaji kubadilishiwa dawa na kupewa ushauri unaostahili.
Mpenzi msomaji, ni vyema tukazidi kuwa makini na kuchukua tahadhari mapema pale tunapoona hali isiyokuwa ya kawaida katika afya zetu.
Chanzo: Tanzlife Company Limited
13 Comments