Articles

MAMBO YA KUKUMBUKA KABLA YA KUTUMIA DAWA

By

on

Mpenzi msomaji, ni siku nyingine tena ambayo kwa mapenzi ya mwenyezi Mungu tumeweza kuiona na hatuna budi kumshukuru Mungu kwa wema wake.

Napenda kuchukua nafasi hii kukuarika wewe ndugu msomaji, ili tuweze kwenda pamoja katika kujifunza na kujikumbusha mambo muhimu mbalimbali yahusuyo afya zetu, mambo muhimu kabisa kuhusu dawa na matumizi yake kwa ujumla.

Katika somo letu la leo tutajifunza au kujikumbushia mambo makuu matatu, mambo hayo ni maana halisi ya dawa, wakati ambao mtu anahitajika kutumia dawa na pia tutajifunza/kujikumbusha kuhusu matumizi salama ya dawa.

Tukianza na kipengele cha kwanza ambacho ni kuhusu maana halisi ya dawa, ndugu msomaji inawezekana kabisa neno dawa siyo mara yako ya kwanza kulisikia, na pindi ulisikiapo tayari kuna picha inayojengeka akilini mwako kuhusu neno au kitu hiki. Dawa ni kitu chochote ambacho asili yake yaweza kuwa ni wanyama, mimea au chembechembe maalumu ambazo zimeandaliwa kitaalamu/kisayansi kwa matumizi ya kuzuia magonjwa, kutibu magonjwa, kuwezesha vipimo mbalimbali vya magonjwa kufanyika au pia kubadilisha mfumo wa utendaji kazi katika mwili. Hiyo ndiyo maana ya dawa.

Kabla ya kuanza matumizi ya dawa, ni vyema kufahamu ni wakati gani mtu anahitajika kutumia dawa. Katika hali ya kawaida hakuna mtu anayependa atumie dawa. Ila katika hili huwa mtu kimsingi analinganisha faida na hasara za kutumia au kutokutumia dawa pindi afya yake inapokuwa siyo imara. Mfano ni faida zipi utapata endapo utaitumia dawa?, ni hasara zipi utapata endapo utaamua kutokutumia dawa?. Baada ya kujiridhisha katika majibu ya baadhi ya maswali kama hayo, ndipo inafika tamati kwamba utumie au usitumie dawa. Pamoja na kujiridhisha katika majibu ya maswali hayo, bado kuna haja ya kufahamu kuwa dawa itatumika tu endapo mtumiaji kulingana na hitaji lake kiafya atatakiwa kutumia ili atatue moja ya mambo yafuatayo ikiwemo, kutumia kwa lengo la kuzuia ugonjwa au kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na ugonjwa fulani, mfano hivi karibuni serikali pamoja na wataalamu wa afya wamekuwa wakielimisha jamii kuhusu matumizi ya dawa aina ya SP (Sulphadoxine/Pyrimethamine) ambayo matumizi yake ni kwa lengo la kuzuia madhara yanayoweza kusababishwa na malaria kwa mama mjamzito. Katika hili, dawa itatumika kwa lengo la kuzuia na siyo kutibu. Ndugu msomaji mfano mwingine ni kuhusu chanjo kama vile chanjo za surua, hutolewa ili kuzuia ugonjwa na siyo kutibu.

Wakati ambapo pia mtu anahitajika kutumia dawa ni katika kutibu. Hii ni baada ya kufahamika kuwa mtu analo tatizo gani kiafya ndipo uamuzi wa kutumia dawa husika unafanywa. Huwezi kuamua kutumia dawa kutibu tatizo usilolifahamu. Inawezekana matumizi ya dawa yakawa hayana manufaa kwako.

Pia kuna wakati daktari wako atakupatia/kukushauri utumie dawa fulani ili kwa namna moja au nyingine iwezekane kukufanyia kipimo fulani na hatimaye aweze kujua tatizo la kiafya ulilonalo na kuamua njia sahihi zaidi ya kuweza kukusaidia.

Wakati mwingine mtu atahitajika kutumia dawa ili kubadili mfumo wa utendaji kazi katika mwili wake. Mfano dawa zinapotumika katika kumlaza mtu na kumfanyia operesheni maarufu kwa jina la dawa za kaputi au nusu kaputi. Pia dawa zinazotumiwa kuongeza nguvu mfano kwa wanamichezo wasiyokuwa waaminifu ili waongeze ufanisi katika kukimbia au katika kushindana kimichezo.

Ndugu msomaji, pamoja na mtu kuhitajika kutumia dawa ni muhimu kufahamu namna bora ya kuitumia dawa ili dawa hiyo iweze kuwa na manufaa kwake kwa kumsaidia kiafya, lakini pia kuitumia bila ya kuleta madhara au kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi mabovu ya dawa hiyo.

Matumizi salama ya dawa yanaanzia na kutumika kwa dawa pale TU inapohitajika. Mtu kutumia dawa wakati haihitajiki ni kujisababishia matatizo yasiyokuwa ya lazima. Kama unalo tatizo ni vyema kupata ushauri wa wataalamu wa afya kabla ya kuanza matumizi ya dawa.

Jambo lingine ni usahihi wa dozi, kama umeshauriwa kutumia kipimo fulani cha dawa basi tumia kipimo hicho. Kinyume na hapo utakuwa aidha umetumia dozi ndogo ambayo haitakusaidia au dozi kubwa ambayo pia itakusababishia madhara makubwa kiafya). Muda wa kutumia dawa pia ni muhimu. Kama ni kila baada ya masaa nane basi iwe hivyo, mfano umeandikiwa dawa aina ya Paracetamol/Panadol vidonge vyenye uzito wa miligramu 500 utumie 2 mara 3. Hii ina maana kwamba siku nzima ina masaa 24 na endapo dawa husika inatakiwa itumike mara tatu inamaana kuwa masaa 24 ya siku nzima, uyagawanye mara 3 ndipo itafahamika kuwa uitumie kila baada ya masaa mangapi. Katika mfano huu, panadol 2 mara 3 maana yake ni kuwa umeze vidonge viwili kila baada ya masaa nane kwani 24 ukigawanya kwa 3 jibu lake ni 8 ambayo ni kila baada ya masaa hayo 8 ndipo umeze dawa hiyo, bila kujali ulianza kuimeza asubuhi, mchana au jioni/usiku.

Urefu wa dozi ni kitu cha kuzingatia katika matumizi salama ya dawa. Endapo umeandikiwa dozi ya siku saba basi itumie dawa kwa siku saba. Kinyume na hapo utasababisha vijidudu vya magonjwa viwe sugu katika dawa na endapo utahitajika siku nyingine kuitumia dawa husika utakuta dawa hiyo haikusaidii tena. Kitaalamu hali hii hujulikana kama Antimicrobial Resistance.

Katika kutumia dawa huwa inaambatana na baadhi ya masharti. Mfano usinywe vinywaji fulani au tumia chakula kabla ya kumeza dawa au usiihifadhi dawa fulani katika eneo lenye joto. Hii husaidia dawa ifanye kazi kwa ufanisi na pia kukupunguzia baadhi ya madhara yasiyokuwa ya lazima, mfano kula chakula kabla ya kumeza dawa aina ya Aspirini (Acetyl Salicylic Acid) vidonge husaidiwa dawa isikwangue au kuunguza tumbo ili usipate vidonda vya tumbo.

Dawa hutumika kulingana na aina ya hitaji la mtu kiafya. Kuna baadhi ya watu wamekuwa wakipeana dawa kwa kuaminishana kuwa wanamatatizo yanayofanana. Inawezekana ni kweli lakini siyo lazima wote kutumia dawa ya aina moja. Mfano wote mnaweza kuwa na tatizo la kuhisi maumivu ya kichwa, mmoja wenu akawa na dawa aina ya Diclofenac vidonge, ukimpatia mwenzako aitumie huwezi kujua ana matatizo gani mengine ya kiafya mfano akiwa na tatizo la Presha ukimpatia naye atumie dawa hii utakuwa hujamsaidia kwani kwa mtu mwenye presha kubwa dawa hii haimfai. Au kupeana Aspirini vidonge kwa mtu mwenye vidonda vya tumbo dawa hii haimfai.

Ndugu msomaji, jambo lingine ni kuhusu aleji ya dawa kwa baadhi ya watu. Kama kuna dawa umewahi kuitumia na ikakuletea madhara ni vyema ukamfahamisha daktari wako kabla hajapendekeza wewe utumie dawa gani kulingana na aina ya tatizo ulilonalo, na pia kama dawa uliyopewa imekusababishia madhara acha kuendelea kuitumia na fika katika kituo cha kutolea huduma za afya kwa msaada zaidi.

Endapo dawa itatumika pindi inapohitajika, na pia ikitumika katika utaratibu unaofaa, itakuwa na manufaa kwa mtumiaji.

Chanzo: Tanzlife Company Limited

 

About Admin

Avatar

Recommended for you