Articles

MATATIZO YA URIC ACID MWILINI

By

on

 

Mwili wa binadamu kwa asili yake umeumbwa kwa namna ambayo viungo vyote vinaweza kufanya kazi kwa ufasaha kutegemeana na taarifa ambazo zinasafirishwa kutoka katika ubongo na kupelekwa katika kiungo husika.

Ili mwili uweze kufanya kazi vizuri na kusitokee na tatizo lolote, haina budi kila kemikali ya asilia iliyopo mwilini iwe katika kiwango ambacho ni stahiki.

Miongoni mwa kemikali asilia ambayo inapatikana katika mwili wa binadamu ni hii ijulikanayo kwa jina la kitaalamu la “Uric Acid”.

Uric Acid ni kemikali ya asilia ambayo inapatikana katika mwili wa binadamu. Kemikali hii hupatikana baada ya kuvunjwa vunjwa kwa vyakula ambavyo ndani yake kuna kundi la kemikali aina ya “Purine” ambayo baada ya kuvunjwa ndipo huzalisha kitu kinachojulikana kama “Uric Acid”.

Katika mwili wa binadamu, kiwango ambacho ni cha kawaida mtu kuwa nacho ni 2.4-6.0 mg/dL (kwa mwanamke) na 3.4-7.0 mg/dL (kwa mwanamme). Kiwango cha uric acid mwilini hupimwa kwa kutumia njia ya damu.

Kiwango hiki endapo kitazidi mwilini kitasababisha matatizo mwilini na hasa katika maeneo ya mwili ambayo ni maungio ya mifupa/jointi.

Katika maungio ya mifupa au jointi, mtu atapatwa na maumivu makali, kuvimba na kubadilika kwa umbile la maungio ya mifupa na kuwa kama kumepinda. Hali hii kitaalamu au ugonjwa hujulikana kama “Gout”.

Pia kuzidi kwa kiwango cha uric acid mwilini kinaweza kuwa ni dalili ya magojwa kama vile magonjwa ya ini, figo pamoja na saratani. Mwilini kemikali hii ya asilia hutolewa kupitia njia ya mkojo kama urea, tofauti na wanyama wengine au ndege ambao wao kemikali hii hutolewa kupitia kinyesi na wakati mwingine imekuwa na muonekano kama chokaa na kuchanganyika na kinyesi mfano cha kuku.

Upatikanaji wa uric acid mwilini ni kupitia ulaji wa vyakula kama vile maharagwe yaliyokaushwa, maini, figo pamoja na baadhi ya vyakula vya baharini au seafood (sardines pamoja na tuna). Pamoja na vyakula, pia uric acid mwilini hupatikana baada ya matokeo ya seli hai za mwili kuvunjika (seli kufa na kutengeneza purine ambazo nazo huvunjika na kutengeneza Uric Acid).

Kwa kuwa kiwango kikubwa cha uric acid kinasababisha matatizo ya kiafya, ni vyema kufahamu ni namna gani ambavyo mtu anaweza kuenenda ili kuhakikisha kuwa kiwango cha uric acid katika mwili kinakuwa siyo cha kuweza kusababisha matatizo ya kiafya.

Miongoni mwa njia za kutumia katika kurekebisha kiwango cha uric acid mwilii ni kuepuka vyakula ambavyo vina kiasi kikubwa cha “Purine” ambayo ndiyo hupelekea kupatikana kwa uric acid. Vyakula hivyo vya kuepuka ni pamoja na maini, figo pamoja na baadhi ya vyakula vya baharini kama vilivyotajwa hapo juu. Pia ni vyema kutumia vyakula ambavyo vina kiasi kikubwa cha virutubisho pamoja na vitamin ambavyo kiafya vinasaidia katika kuondoa sumu mwilini.

Virutubisho na vitamini ambazo husaidia katika kurekebisha kiwango cha uric acid mwilini ni pamoja na vitamin B6, Vitamin C, madini ya magnesium. Haya hupatikana katika matunda kama vile ndizi mbivu, machungwa, matikiti maji, maembe pamoja na mananasi. Pia juisi la limao katika mwili husaidia katika kutengeneza chumvi aina ya calcium carbonate ambayo husaidia kuyeyusha au (Neutralize) tindikali asilia mwilini (Uric acid).

Aidha, sambamba na ulaji wa vyakula hivyo kwa mtu ambaye tayari analo tatizo la kuwa na kiwango kikubwa cha uric acid mwilini (Baada ya vipimo vya kitaalamu), inashauriwa kutumia dawa ambazo hupunguza kuzalishwa kwa uric acid mwilini lakini pia kusaidia katika kuondoa maudhi na maumivu makali ambayo mtu huyapata katika jointi. Moja na dawa ambazo zimekuwa zikitumika katika tatizo hili ni dawa aina ya Allopurinol.

Ili miili yetu iweze kuendelea kufanya kazi vizuri, inashauriwa kufanya chunguzi za kitaalamu ili kuweza kubaini mapungufu yaliyopo mapema na hatimaye kuepukana nayo kwa kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.

Chanzo: Tanzlife Company Limited

About Admin

Avatar

Recommended for you

4 Comments