Ugonjwa wa kisukari ni tatizo la kiafya ambalo mwili wa binadamu unashindwa kutawala kiwango cha sukari ambacho kinatakiwa kuwa katika mzunguko wa damu na mwili kwa ujumla.
Mwili unaposhindwa kutawala kiwango hicho husababisha sukari kuongezeka katika damu na hatimaye kuharibu mifumo ya mwili kufanya kazi inavyopaswa.
Ugonjwa huu ni moja ya magonjwa ambayo yapo katika kundi la magonjwa yasiyoambukiza. Magonjwa yasiyoambukiza ni yale ambayo mtu anaweza kuyapata kwa kutegemeana na staili za maisha alizonazo mtu mfano ulaji, vinywaji au pia inawezekana likawa ni tatizo ambalo mtu anazaliwa nalo.
Kutegemeana na chanzo cha ugonjwa huu wa kisukari, (Diabetes type I, and Diabetes type II), matibabu yake yanahusisha dawa mbalimbali ambazo kwa pamoja husaidia kurekebisha kiwango cha sukari kwa mtu mwenye tatizo hili.
Tatizo la kisukari kutegemeana na ukubwa wake, linaweza kupelekea mtu apate matatizo mengine yakiwemo vidonda vinavyochelewa kupona, kuharibika kwa mishipa ya damu, matatizo ya nguvu za kiume, pamoja na magonjwa ya moyo.
Hali hii husababisha matibabu kwa mgonjwa kuhusisha dawa mbalimbali ambazo zitasaidia kutibu matatizo hayo mengine ambayo chanzo chake kimekuwa ni tatizo la kisukari.
Miongoni mwa dawa zinazotumika moja kwa moja katika kutibu tatizo la kisukari ni pamoja na dawa ya sindano (Insulin) na dawa za vidonge (Mfano Glibenclamide na Metformin).
Dawa ya sindano aina ya Insulin, ni dawa ambayo imetengenezwa kutoka katika chembechebe asilia zinazopatikana kwa wanyama. Ili dawa hii iweze kumsaidia mgonjwa ni lazima itumike kulingana na dozi ambayo mgonjwa ameandikiwa na daktari, pia kwa kuwa mgonjwa anaweza kupatiwa ili aweze kuitumia akiwa mazingira ya nyumbani, kitu cha msingi cha kukumbuka ni kuwa uhifadhi wa dawa hii ni katika mazingira yenye ubaridi mfano katika friji (haitakiwi kuigandisha). Aidha kwa mazingira ambayo hakuna friji, mgonjwa anashauriwa kuihifadhi kwa kuiweka katika chombo/mkebe na kuitumbukiza katika maji yenye ubaridi. Dawa hii haitokuwa na msaada katika matumizi endapo itahifadhiwa katika mazingira yenye joto mfano kabatini, jikoni au dirishani ambapo mionzi ya jua inapita muda mwingi.
Katika matumizi ya dawa jamii ya vidonge, mambo ya msingi ya kukumbuka pamoja na usahihi wa dozi ni kuhakikisha kuwa dawa uliyopewa na mtaalamu wa afya unaitumia katika ratiba sahihi ya ulaji wa chakula, je unatakiwa kuitumia kabla au baada ya chakula?. Tukumbuke ya kuwa vyakula tunavyokula siku zote vinachangia kuongea nguvu/sukari na joto mwilini (Vyakula vyenye wanga). Hivyo dawa inayotumika inatakiwa ikasaidie kupunguza kiwango cha sukari ambacho kitaingia mwilini kutoka katika chakula cha wanga ambacho kimetumika au vinywaji.
Mfano dawa aina ya Metformin vidonge, hutumika kwa mgonjwa wa kisukari ambaye seli za mwili wake zinashindwa kuhisi (sense) uwepo wa insulin(asilia katika mwili ambayo hurekebisha kiwago cha sukari). Matumizi ya dawa hii ni kuboresha uwezo wa mwili katika kurekebisha kiwango cha sukari katika damu. Katika kuitumia inashauriwa dawa hii itumike pamoja na chakula.
Kutegemeana na hali ya mgonjwa, kuna mazingira ambapo dawa zote mbili (Vidonge na sindano) zikatumika kwa pamoja ili kumsaidia mgonjwa.
Wakati mgonjwa anatumia dawa za kisukari, mfano kwa mgonjwa anayetumia dawa aina ya metformin ni vyema akachukua tahadhari katika matumizi ya dawa hizi, furosemide (lasix), nifedipine (dawa ya presha), cimetidine/ranitidine(dawa za vidonda vya tumbo na kiungulia) pamoja na digoxin (dawa ya moyo).
Kwa kuwa ugonjwa wa kisukari pia unaweza kumsababisha mtu kupatwa na vidonda ambavyo havitibiki kwa urahisi, inashauriwa mgonjwa kuwa mwangalifu katika kujilinda asipatwe na majeraha, aidha endapo majeraha yatatokea, huduma ya dawa/matibabu itategemeana na uchunguzi wa kitaalamu. Aidha kuna dawa za kupakaa ambazo mgonjwa anaweza kupatiwa ili ziweze kumsaidia katika kutibu vidonda.
Pia kisukari kinaweza kusababisha matatizo ya nguvu za kiume, endapo mgonjwa wa kisukari atapatwa na hali hii ni vyema akamfahamisha daktari ili aweze kumsaidia kwa kumpatia dawa na ushauri unaofaa ili aweze kuondokana na hali hiyo.
Pamoja na matumizi ya dawa katika kutibu kisukari, inashauriwa kufuata kanuni za afya mfano kufanya mazoezi na kuwa na ulaji mzuri/salama wa vyakula na vinywaji ili tuweze kuendelea kuilinda afya.
Chanzo: Tanzlife Company Limited