Articles

MATUMIZI YA DAWA YA ASPIRIN KWA WAGONJWA WENYE PRESHA YA KUPANDA

By

on

Katika historia ya matumizi ya dawa na huduma za matibabu ya binadamu kwa ujumla utakubaliana na mimi kuwa, miongoni mwa dawa ambazo zimekuwa zikitumika tangu enzi na enzi ni dawa ijulikanayo kwa jina la Aspirin.

Dawa hii ikiwa hivi sasa ni zaidi ya miaka mia moja inatumika, imekuwa msaada mkubwa sana katika kuimarisha afya za wanadamu. Jina hili la Aspirin ni jina la kibiashara ambapo kwa kitaalamu dawa hii hujulikana kama acetylsalicylic acid.

Mpenzi msomaji inawezekana ukawa ni mmoja wa ambao wamewahi kuitumia dawa hii aina ya Aspirin, ama kwa kuandikiwa na daktari au kwa matumizi binafsi pasipo kuandikiwa ama kushauriwa na wataalamu wa afya. Lakini, kwa matumizi yaliyozoeleka na watu wengi ni kuitumia dawa hii kwa malengo ya kuondoa maumivu ya mwili mfano maumivu ya kichwa na viungo vingine katika mwili.

Pia dawa hii imekuwa ikitumika katika kushusha homa na kusaidia eneo lenye jeraha au uvimbe liweze kurejea katika hali yake ya uzima na kuweza kufanya kazi kwa ubora zaidi. Kwa kitaalamu matumizi hayo yamegawanywa katika sehemu tatu ambapo ni kuzuia maumivu (Anti pain or Analgesic), kushusha homa (Antipyretic) na tatu ni kusaidia katika uvimbe na majeraha (Anti inflammatory).

Pamoja na matumizi hayo hapo juu ya dawa hii ya Aspirin, dawa hii inazo sifa ambazo huiwezesha kuwa msaada mkubwa kwa wagonjwa na watu walio katika hatari ya kupata shinikizo la damu au presha ya kupanda.

Miongoni mwa vitu ambavyo humfanya mtu apate presha ya kupanda ni pamoja na kuongezeka kwa ujazo wa damu mwilini, mishipa ya damu kuwa miembamba kutokana na mwili kuongezeka au kuta za mishipa ya damu kuwa na mafuta, uzito wa damu kuongezeka na sababu nyinginezo ikiwemo msongo wa mawazo.

Katika sababu tajwa hapo juu zinazopelekea mtu kupata presha ya kupanda, dawa ya Aspirin husaidia sana katika kuiwezesha damu isiwe nzito kwa kuzuia mgandamano wa seli katika damu (inhibits platelet aggregation). Endapo seli zitagandamana katika damu, zitaisababisha damu iwe nzito na hivyo kuifanya presha ipande. Aidha, kutokana na damu kugandamana kutapelekea hatari ya kutokea tatizo la kiharusi (stroke) na hivyo kuhatarisha zaidi uhai wa mgonjwa. Seli zilizogandamana zinaweza kusafiri na kukwama katika mirija ya damu na hivyo kuzuia sehemu nyingine katika mwili isipate mawasiliano pamoja na damu kwa ujumla.

Ili kuweza kuepukana na tatizo la presha ya kupanda pamoja na hatari ya kupata tatizo la kiharusi, ni vyema ukapima afya yako sasa. Kiasi au dose ya dawa ya aspirin ambayo itakufaa kutumia itafahamika mara baada ya kuonana na daktari na kukufanyia uchunguzi wa kutosha.

Mpenzi msomaji pamoja na umuhimu wa dawa ya Aspirin kwa wagonjwa wenye presha ya kupanda, pia zipo tahadhari za kuchukua kabla ya kuitumia dawa hii. Tahadhari hizo ni pamoja na hizi zifuatazo:

Dawa hii haishauriwi kutumiwa na mtu ambaye anayo historia ya kutokwa na damu mara kwa mara, mtu mwenye aleji na mchanganyiko wa dawa hii, mtu aliye na vidonda vya tumbo, mtu anayetumia dawa za kuzuia seli za damu kugandamana. Pia, sababu za kutotumia dawa hii itategemeana na namna uchunguzi wa daktari utakavyo kuwa.

Katika kuzuia presha ya kupanda, tuendelee kuzingatia kanuni za afya zinavyotuelekeza. Pia, matumizi salama ya dawa ya Aspirin husaidia katika kupambana na tatizo hili.

Chanzo: Tanzlife Company Limited

About Admin

Avatar

Recommended for you