Articles

MOSHI WA SIGARA KWA WATOTO NA WAJAWAZITO

By

on

SIGARA

SIGARA

Watoto na wajawazito ni miongoni mwa makundi katika jamii zetu ambayo yanapewa uangalizi wa karibu sana. Ili watoto waweze kukua vizuri na pia kwa wamama wajawazito kuweza kujifungua watoto wenye afya bora, ni vyema pia swala la hewa inayovutwa na watu hawa ikawa na usalama wa kutosha.

Pamoja na uvutaji wa sigara na moshi wake kuwa na madhara ya kiafya kwa watu wote, napenda kuchukua nafasi hii kukushirikisha na uweze kukumbuka au kuyafahamu madhara yanayopatikana kwa watoto kuvuta hewa iliyo na moshi wa sigara na pia madhara ya uvutaji wa sigara kwa wamama wajawazito.

Kabla ya kukufahamisha madhara yanayoletwa na sigara au moshi wake, tuangalie kwanza ni kemikali gani ambazo zinapatikana katika sigara au moshi wake. Katika moshi wa sigara baadhi ya kemikali zinazopatikana ni zifuatazo: Nicotine, Carbon monoxide, Arsenic, Ammonia, Hydrogen Cyanide, Benzene pamoja na Vinyl chloride.

Kwa mama mjamzito anayevuta sigara au ambaye yupo katika mazingira ya moshi wa sigara (Anavuta sigara bila kujifahamu au bila lidhaa yake), husababisha madhara yafuatayo kwa mtoto aliyeko tumboni:

Upungufu wa hewa ( Oxygen) kwa mtoto tumboni, hii husababishwa na kemikali (Carbon monoxide) ambayo hupunguza na kuzuia damu isibebe oxygen, hivyo mtoto tumboni anakosa hewa ya kutosha na kumsababishia matatizo katika ukuaji wake wa ubongo, hii pia hupelekea mtoto kuzaliwa akiwa na matatizo ya akili.

Mtoto kuzaliwa akiwa na matatizo au hatari ya kupata magonjwa ya moyo, hii husababishwa na kemikali (Nicotine) ambayo hupenyeza katika mfuko wa uzazi (Placenta) na kumfikia mtoto, husababisha mishipa yake ya damu kuwa miembamba zaidi na hivyo kumfanya apate au awe katika hatari ya kupata magonjwa ya moyo.

Mtoto kuzaliwa akiwa na uzito mdogo kuliko kawaida (chini ya kilo mbili na nusu), hii husababishwa na mtoto kukosa hewa ya kutosha pamoja na sumu tofauti tofauti zilizoko katika moshi wa sigara kumuathiri ukuaji wake.

Pia husababisha mama mjamzito kupata matatizo mbalimbali yanayohusiana na ujauzito, (Pregnancy complications).

Kuwa jirani na mtu anayevuta sigara, inamaanisha wewe unaivuta ile sigara bila kujifahamu (Secondhand smoke), fikiria mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja yupo mazingira ya moshi wa sigara, labda ni baba, mama au mtu yeyote anavuta sigara karibu na mtoto mdogo……kwa watoto wadogo, moshi wa sigara unayo madhara yafuatayo:

Watoto wadogo, viungo vya miili yako ni vichanga bado, mfano mapafu au mfumo wa upumuaji, moyo, ini na viungo vingine, moshi wa sigara humfanya mtoto awe katika hatari ya kupata magonjwa ya mfumo wa upumuaji kama vile pumu, neumonia (pneumonia), pia kwa muda mrefu huongeza hatari ya mtoto kupata magonjwa ya kansa, magonjwa ya moyo, magonjwa ya masikio pamoja na macho.

Inawezekana kuvuta sigara ni jambo la lazima kwako, basi usivute sigara karibu na mama mjamzito, watoto wadogo, mama mjamzito epuka sigara au moshi wake ili kumlinda mtoto aliyeko tumboni, pia ni ustaarabu mzuri kutovuta sigara maeneo yenye mkusanyiko wa watu (Public Areas).

Chanzo: Tanzlife Company Limited

 

 

 

About Admin

Avatar

Recommended for you