Articles

MTOTO MMOJA KUWA NA MAMA WAWILI HALALI, INAWEZEKANA

By

on

MTOTO MMOJA, MAMA WAWILI HALALI

MTOTO MMOJA, MAMA WAWILI

Katika mazingira ambayo tumeyazoea kuhusiana na mambo ya uzazi ni kuona, mama mmoja na baba mmoja kuwa wazazi halali wa mtoto, au kwa lugha ya kitaalamu wanasema, one biological mother and one biological father. Hivi ndivyo watu tulivyozoea kusikia kwamba mtoto mmoja hawezi akawa na mama wawili au mtoto mmoja hawezi akawa na baba wawili, labda wawe ni wa kufikia.

Ulimwengu wa sayansi kila siku unakuwa na kubadilika, na wakati mwingine mambo yanayotokea katika sayansi, ni vigumu kuelezeka katika lugha ya kawaida, ila ndivyo utashi au maarifa ya mwanadamu yanavyobadilika au kukua.

Mpenzi msomaji, tutakumbuka kwamba ujauzito kwa mwanamke ni matokeo ya muunganiko wa mbegu za kiume (sperms) pamoja na yai kutoka kwa mwanamke. Muunganiko au kurutubishwa (fertilization) kwa yai la mwanamke na mbegu za mwanaume ndiko hupelekea ujauzito au mtoto apatikane.

Siku zote, kurutubishwa huku kwa yai la mwanamke hutokea katika mirija ya uzazi ya mwanamke (fallopian tube) na baadae yai hili lililorutubishwa husafiri mpaka kwenye mji wa mimba, maendeleo yote na kukua kwa ujauzito hutokea hapo mpaka muda wa mwanamke kujifungua unapofika.

Katika hali ambayo yawezekana ikawa siyo ya kawaida, yai huweza kurutubishwa nje ya mwili wa mwanamke kwa njia za kibaiolojia, in-vitro fertilization (IVF), kurutubishwa huku hufanyika kwa kuchukua yai la mwanamke na mbegu za mwanamme na kisha kuviunganisha maabara.

Sayansi hii ya kurutubisha yai maabara imekuwa ikitumiwa kwa muda sasa, na miongoni mwa sababu za kuitumia ilikuwa ni mambo ya tafiti za kisayansi, baadhi ya wanawake kushindwa kubeba ujauzito na hivyo kuamua kutoa yai ili lirutubishwe maabara waweze kupata mtoto, baadhi ya magonjwa kwa wanawake yanayomfanya ashindwe kubeba ujauzito na hivyo kuamua kuchukua uamuzi huu, ila pia kwa baadhi ya wanawake wanajikuta kila wakibeba ujauzito, unatoka, hivyo njia ya kufanya ili wapate watoto wamekuwa wanatumia njia hii ambayo kwa ujumla siyo ya gharama kidogo, ni bei ghali karibu zaidi ya milioni 100 za kitanzania.

Baada ya yai kurutubishwa maabara , inawezekana likapandikizwa kwa mwanamke yeyote yule ambaye anaweza kubeba ujauzito, na hapa ndipo inaleta uwezekano wa wanawake wawili kuwa wazazi halali wa mtoto mmoja.

Mpenzi msomaji, katika nchi zilizoendelea, swala la kupata mtoto wa kufikia au nisema, adoption, ni swala gumu kwa sasa, hivyo inatokea mwanamke anayo mayai, ila hana uwezo wa kubeba ujauzito, au vyote anavyo ila hahitaji kubeba ujauzito. Kinachofanyika ni wanawake kukubaliana juu ya hili, mwanamke mmoja anakubali kutoa yai lake, linarutubishwa maabara kwa mbegu za mwanamme wanayehitaji awe baba wa yule mtoto, na kisha linapandikizwa kwa yule mwanamke mwingine ambaye yeye atakuwa na jukumu la kubeba ujauzito. Hivyo mwanamke mmoja atakuwa ametoa yai, na mwingine atakuwa anabeba ujauzito, kibaiolojia wanawake wote hawa wawili ni mama halali wa mtoto atakayekuja kuzaliwa.

Mpenzi msomaji, jambo hili la wanawake kuwa wazazi halali wa mtoto mmoja limechukua sura tofauti pia, kwani wanawake wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja, wanaitumia nafasi hii kupata watoto, wanachokifanya ni kuamua, wewe utaibeba mimba ya mtoto wa kwanza, na wewe utaibeba mimba ya mtoto wa pili.

Hivi ndivyo ulimwengu wa kibaiolojia unavyobadilika siku hadi siku, je swala hili unalionaje?, wewe ndiye msemaji.

Mpenzi msomaji, nia na madhumuni ya Blog hii ni kukufahamisha na kukuelimisha juu ya mambo mbalimbali yanayohusiana na afya, na pia kukupatia wewe msomaji nafasi ya kukutana na wadau au watu mbalimbali ili kuweza kubadilishana maarifa na uzoefu juu ya mambo ya afya kupitia ukurasa wetu wa Facebook kwa kui LIKE Page yetu ya Tanzlife, kwa kutufuata katika Twitter, @tanzlife na pia kupitia Health Forum katika Website hii ya Tanzlife. Endelea kupata taarifa au elimu ya afya kupitia Website/Blog hii ya Tanzlife.

TUNAWASHUKURU NINYI NYOTE

Chanzo: Tanzlife Company Limited

About Admin

Avatar

Recommended for you