Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Jakaya Kikwete anatarajia kufungua mkutano wa kitaifa wa uzazi wa mpango utakaoanza Oktoba 9 hadi 11 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Charles Pallangyo, ilisema katika mkutano huo, Rais Kikwete pia atazindua nyota ya kijani ya uzazi wa mpango yenye ujumbe mahsusi wa “FUATA NYOTA YA KIJANI, UPATE MAFANIKIO”.
Alisema mkutano huo umeandaliwa kwa kushirikiana na Wadau wa Uzazi wa Mpango nchini na kwamba dhima ya mkutano huo ni “kupata ufumbuzi wa changamoto tulizo nazo ili kusukuma mbele jitihada za kuboresha huduma za uzazi wa mpango”.
“Madhumuni ya mkutano huu ni kutoa fursa ya kufahamishana matokeo ya tafiti zilizofanyika na kubadilishana uzoefu kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu uzazi wa mpango na pia kukubaliana kuhusu mipango ya baadaye ya kuendeleza na kuboresha huduma hizi,”alisema Pallangyo.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, mkutano huo utahudhuriwa na washiriki 520, wakiwemo wawakilishi kutoka Mikoa na Wilaya mbalimbali za Bara na Visiwani.
Pia mkutano huo utahudhuriwa na wageni waalikwa kutoka nje ya nchi. Washiriki wengine ni Watafiti, wawakilishi wa Asasi za Kiraia Mashirika yasiyo ya Kiserikali na watu binafsi.
Mkutano huo unawaweka pamoja watendaji na watafiti ili waweze kujadiliana kuhusu njia muafaka za utekelezaji kwa kutilia maanani mbinu na mikakati inayoweza kuboresha huduma za uzazi wa mpango.
Pia watajadili mikakati itakayosaidia katika kupanua wigo wa huduma za uzazi wa mpango ili kufikia lengo la Taifa.
Mkutano huo wa Kitaifa wa Uzazi wa Mpango ni matokeo ya mkutano wa Kimataifa wa Uzazi wa Mpango uliofanyika mjini London nchini Uingereza mwezi Julai, 2012, ambao ulitoa changamoto kwa dunia nzima kuhusu umuhimu wa kuongeza kiwango cha watumiaji wa huduma ya uzazi wa mpango kwa hiari katika nchi 69 zinazoendelea.
Katika mkutano huo wa London, nchi kadhaa ikiwemo Tanzania, Wadau wa Asasi za Kiraia kutoka duniani kote ziliazimia kuongeza jitihada ili kufikia lengo la Kimataifa la kuwafikia akinamama na wasichana 120 milioni wenye mahitaji mbalimbali ya uzazi wa mpango ifikikapo mwaka 2020.
Mkutano huo wa kitaifa pia utatoa fursa kwa wadau wa uzazi wa mpango nchini kuweka maazimio yatakayosaidia katika kuinua kiwango cha uzazi wa mpango.
Wawakilishi toka ngazi mbalimbali za Serikali (kuanzia ngazi ya Taifa, Mikoa na Wilaya), wawakilishi toka Asasi za Kiraia, Wadau wa Maendeleo na Sekta ya watu binafsi wataweka maazimio yatakayowezesha kupanua wigo wa huduma za uzazi wa mpango kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 27 na kufikia lengo la Taifa la asilimia 60 ya watumiaji wa njia za kisasa za uzazi wa mpango ifikapo 2015.
Mkutano huo wa uzazi wa mpango utawawezesha washiriki kukubaliana jinsi ya kuboresha huduma kwa kutilia maanani changamoto zilizopo, uzoefu uliopatikana na fursa zilizopo ili kupata njia zifaazo zaidi katika kuboresha huduma za uzazi wa mpango nchini.
Chanzo: Tanzlife Company Limited