Articles

SABABU ZA MWANAMKE KUSHINDWA KUPATA UJAUZITO

By

on

Moja ya matatizo yaliyoko katika jamii zetu na yamesababisha wanandoa wengi au wanawake wengi kukosa furaha, ni kukosa uwezo wa kupata ujauzito kwa mwanamke.

Sote tunafahamu kuwa, swala la mwanamke kupata ujauzito linahusisha pande zote mbili, yaani upande wa mwanamke na pia upande wa mwanamme, wote wawili wanapokuwa katika afya nzuri ndipo ujauzito unaweza kupatikana kwa mwanamke.

Miongoni mwa sababu zinazoweza kumfanya mwanamke ashindwe kupata ujauzito ni kama zifuatazo:

Matatizo katika homoni, hii ni kutokana na kwamba, mzunguko (Menstrual cycle) katika mwili wa mwanamke hutawaliwa na hizi kemikali asilia ndani ya mwili ambapo mabadiliko madogo yakitokea katika uzalishaji wa hizi homoni au homoni kuzalishwa katika wakati ambao siyo muafaka huweza kupelekea mwanamke akashindwa kupata ujauzito, pia tatizo la kuwa na uzito wa mwili mdogo sana au mkubwa sana pia huathiri hali nzima ya homoni na kupelekea kushindwa kupata ujauzito.

Umri, kwa wanawake uwezo wa kupata ujauzito unapungua kwa kadri umri unavyoongezeka, hii inatokana na kupungua kwa uzalishaji wa homoni husika wakati umri unavyoongezeka. Kuanzia miaka 35 na kuendelea huwa kunakuwa na tatizo la kushindwa kupata ujauzito kwa wanawake wengi.

Kuziba kwa mirija (fallopian tubes), hii husababisha mbegu za kiume (sperms) zishindwe kulifikia yai na kulirutubisha ili ujauzito utokee. Kuziba kwa mirija huweza kusababishwa na magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya kujamiiana, matatizo katika kizazi au upasuaji. Mara nyingi wanawake ambao mirija yao imeziba, hawahisi dalili zozote.

Ute ute katika kizazi (mucus problems), ute unaopatikana katika kizazi cha mwanamke huwa na sifa ya kuruhusu mbegu za kiume ziweze kusafiri kwa urahisi na kulifikia yai ili kulirutubisha. Kwa baadhi ya wanawake ute huu unakuwa na uzito na kemikali ambazo ni vigumu kwa mbegu za kiume kuweza kupita, na wakati mwingine mwili wa mwanamke huzalisha sumu ambazo huziua mbegu za kiume, haya yote husababisha kukutana kwa yai na mbegu za kiume kusitokee na hivyo ujauzito kutopatikana.

Uvimbe katika kizazi (fibroids), hii huchangia asilimia tatu (3%) katika mwanamke kutopata ujauzito. Uvimbe huu ambao hutokea katika kuta za mji wa mimba, kwa namna moja au nyingine huweza kuzuia yai lililorutubishwa lisikae sehemu yake na hivyo kuathiri kizazi.

Matibabu ya kansa, kwa kutegemeana na aina ya matibabu, aina ya dawa au njia ya mionzi, hizi huweza kumuathiri mwanamke na kumsababishia kushindwa kupata ujauzito.

Ukomavu katika kizazi, kwa baadhi ya wanawake wanayo matatizo ambayo kizazi chao huwa hakijakomaa vizuri au katika kuzaliwa kwao walizaliwa na tatizo hili ambalo, kizazi hakiko sawa (abnormally developed uterus).

Asilimia kubwa ya matatizo ya mwanamke kushindwa kupata ujauzito yanayo tiba, kama unalo tatizo katika kupata ujauzito usikate tamaa, onana na wataalamu wa afya ili uweze kujua chanzo cha tatizo lako na kupatiwa msaada unaostahili.

Chanzo: Tanzlife Company Limited

 

 

About Admin

Avatar

Recommended for you

2 Comments