Articles

TFDA KUCHUNGUZA MAFUTA YA ALIZETI

By

on

DSC00236

 

 Mkaguzi wa Vyakula kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) John Mwingira (kulia) akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu kuendeleza wajasiriamali wadogo wadogo wa bidhaa za chakula. Kushoto ni Ofisa Uhusiano wa mamlaka hiyo Gaudensia Simwanza.

Dar es Salaam

Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imeanza kufanya utafiti wa mafuta ya Alizeti kwa wasindikaji wadogo katika mkoa wa Singida ili kujua ubora na usalama wake.
Mkoa wa Singida ni miongoni mwa mikoa inayozalisha kwa wingi mafuta ya Alizeti lakini wasindikaji wengi wamekuwa hawatumii teknolojia zinazotakiwa kwenye usindikaji.
Kulingana na TFDA mafuta mengi ya Alizeti yanayozalishwa na wasindikaji wadogo wadogo hayajasafishwa kutokana na wasindikaji hao kushindwa kukidhi gharama za teknolojia ya kusafishia mafuta hayo.
Akizungumza leo, Mkaguzi wa Vyakula kutoka TFDA, John Mwingira, alisema gharama ya chini ya mtambo wa kusafishia mafuta hayo ni Dola za Marekani 120 milioni.
“Tulizungumza na Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) na hivi sasa wako kwenye hatua za kutengeneza teknolojia inayofanya kitu kile kile lakini itapatikana kwa gharama nafuu ili wasindakaji waweze kuutumia,”alisema Mwingira.
Kwa mujibu wa Mkaguzi huyo, kupitia mpango huo wa majaribio ya utafiti wasindikaji hao watapatiwa elimu itakayowasaidia kubadilisha mitazamo yao dhidi ya vyombo vya udhibiti.
Hata hivyo alisema katika matokeo ya awali wamebaini kuna tatizo kwenye viwango vya ubora hasa kwenye rangi, harufu na ladha lakini kwenye afya ya binadamu havina shida.
Pia alisema wamekuwa wakiwahamasisha wasindikaji hao wajiunge kwenye vikundi ili kuweza kuunganisha nguvu na kununua mtambo huo kutoka SIDO. Inaelezwa kuwa wastani wa mtaji kwa kila msindikaji mdogo ni Sh5 milioni.
Awali Ofisa Uhusiano wa TFDA, Gaudensia Simwanza, alisema wanaendelea kufundisha wajasiriamali wadogo wa vyakula ili kujua sheria, kanuni na miongozo inayohusu usindikaji wa vyakula.
Kwa mujibu wa Ofisa huyo, hadi sasa wajasiriamali 417 katika kanda zote nchini, za Dar es Salaam, Mbeya, Ziwa, Kaskazini na Kati wamepatiwa mafunzo hayo.
Chanzo: Tanzlife Company Limited

About Admin

Avatar

Recommended for you