Articles

UGONJWA WA KIFAFA NA VIHATARISHI VYAKE

By

on

Kifafa ni ugonjwa unaosababishwa na matatizo katika mifumo ya fahamu ya mwili na siku zote umekuwa unaambatana na dalili za mtu kuanguka huku akitetemeka na mara nyingine hutokwa na povu mdomoni, kutokwa na haja ndogo (mkojo) pasipo kujielewa na pia kung’ata midomo (lips) au ulimi.

Chanzo cha ugonjwa huu hakijafahamika zaidi kitaalamu ila miongoni mwa vihatarishi au mambo yanayoweza kumfanya mtu apate ugonjwa huu ni pamoja na, kuwa na historia ya kifafa katika familia( Kurithi), matatizo ya mishipa ya damu katika ubongo, maambukizi katika ubongo mfano homa ya uti wa mgongo (meningitis), mtoto kuzaliwa kabla ya umri wake, ajari mbaya katika eneo la ubongo, kukosekana kwa hewa ya kutosha katika ubongo, mtoto kupatwa na degedege mara kwa mara katika miezi ya mwanzo ya kuzaliwa kwake, uvimbe katika ubongo na sababu nyinginezo.

Pamoja na visababishi hivyo hapo juu, wakati mwingine kumekuwepo na vitu vinavyochochea mtu apatwe na dalili hizo (kuanguka kifafa), mfano wa vichochezi ni pamoja na kutokula vizuri ( uhaba wa chakula), hali ya hewa, msongo wa mawazo pamoja na mazingira yenye kelele.

Utambuzi wa kifafa hufanyika kitaalamu kwani siyo kila mtu anayeanguka na kutetemeka anaumwa kifafa, inawezekana likawa ni tatizo lingine. Kwa kuonana na wataalamu utambuzi utafanyika.

Mtu mwenye kifafa mara nyingi anakumbwa na changamoto mbalimbali katika jamii anayoishi, kutengwa katika shughuli mbalimbali, wengine wanapatwa na ulemavu baada ya kuanguka na kuumia, lakini pia kutokana na kuona aibu au kuogopa kutengwa wapo wanaokosa matibabu au msaada na mwisho kujikuta wanatumia muda mrefu na gharama kubwa zaidi kujitibu.

Mpenzi msomaji, siku zote ukigundua tatizo, tayari unapata mwanga au sehemu ya kuanzia katika kulitatua tatizo husika. Wahi kwa wataalamu waliopo Jirani yako na chukua tahadhari inapobidi katika kujiepusha na magonjwa.

Chanzo: Tanzlife Company Limited

About Admin

Avatar

Recommended for you