Articles

UJUE UKWELI KUHUSU MSWAKI NA KINYWA CHAKO

By

on

Kinywa na Meno

Usafi wa Kinywa na Meno

Siku zote na mara kwa mara tumekuwa tunatumia miswaki katika kukisafisha kinywa. Miswaki ipo ya aina mbalimbali, ipo ya plastiki, iliyotokana na miti na pia ipo ya kutumia umeme (Electric Toothbrush) na mingine mingi.

Katika kukisafisha kinywa, kila mtu anafahamu namna anavyokisafisha kinywa chake, mambo anayoyafanya kabla na baada ya kutumia mswaki wake na pia utunzaji wa mswaki wake. Katika mswaki na kinywa, leo kunabaadhi ya mambo ambayo ninapenda tukumbushane.

Katika mwili wa binadamu, hii ni pamoja na katika vinywa vyetu, siku zote huwa na wadudu (bacterias) maelfu kwa maelfu wa aina mbali mbali, wapo wadudu wanaosababisha magonjwa na pia wale ambao ni salama katika miili yetu, kadharika na katika mazingira yetu, katika hewa na vingine vyote vinavyotuzunguza pia huwa na wadudu mbalimbali.

Pamoja na kuwepo wadudu hawa katika mazingira na pia katika miili yetu, mtu atapata magonjwa endapo uwiano kati wa wadudu wanaosababisha magonjwa na wadudu ambao ni salama utabadilika kwa maana ya mwili ukiwa na wadudu wengi wanaosababisha magonjwa na pia endapo kinga yake ya mwili (Immunity) yake ikishuka, ndipo atakapopata ugonjwa.

Tafiti zinaonyesha kuwa, mswaki ulioachwa wazi, hubeba mamia kwa mamia ya wadudu (bacterias) wakiwemo wale wasababishao kuharisha, E. Coli, wasababishao magonjwa ya ngozi, Staphylococci na wengine wengi. Hii inamaana kwamba, kila unapotumia mswaki kuna aina fulani ya wadudu (bacterias) unaowaweka katika kinywa chako, pia kuna wadudu unaowarudisha katika kinywa chako kwani kama tulivyoona hapo awali kuwa, katika mwili (kinywa) siku zote wadudu wapo. Hivyo unapoutumia mswaki kuna wadudu unaowatoa na kuwaweka katika mswaki, unapokuja kuutumia mswaki wako tena unawarudisha wale ambao tayari ulikuwa unao. Hii ni sababu mojawapo inayochangia kuwepo kwa magonjwa ya kujirudiarudia ya kinywa/meno. Ila mwili siku zote unayo kinga na uwezo wa kujilinda, ugonjwa utatokea endapo kinga yako itashuka au endapo mswaki mmoja utatumiwa na mtu zaidi ya mmoja.

Wewe ndiye unayefahamu mswaki wako unauhifadhi wapi, tafiti zinaonyesha kuwa chombo cha kuhifadhia mswaki (Toothbrush Holders) kinashika nafasi ya tatu kwa uchafu ndani ya nyumba, hii inatokana na kutopewa umakini wa kutosha pindi usafi unapofanyika nyumbani. Pia watu huhifadhi miswaki yao ndani ya bafu au (washrooms), pindi unapo fanya usafi wadudu (bacterias) husambaa hewani na kubaki katika mswaki. Kwa nini vyombo tunavyotumia kuandaa vyakula au vinywaji, sahani au glasi hatuvihifadhi chooni/bafuni lakini mswaki tunao utumia kinywani tunauhifadhi chooni/bafuni?.

Baadhi ya mambo tunayopaswa kukumbuka ni kuuosha mswaki kwa maji ya kutosha pindi tunapomaliza kusafisha kinywa/meno, kuutunza sehemu ambapo utakauka kwani wadudu wengi hupenda na huzaliana sana kwenye mazingira yenye unyevu, uhifadhi kwa kuusimamisha (sehemu yenye brashi iangalie juu), unaweza kutumia kifaa maalumu kuukausha na kuwauwa wadudu (Toothbrush Sanitizers), usiutumie mswaki mmoja zaidi ya miezi mitatu au minne (ule unaotumia umeme badili brashi) pia tuendelee kuwa na mazoea ya kutunza kinywa na kutumia dawa za kusukutua (antibacterial mouthwash) ili kupunguza wadudu mdomoni kabla ya kupiga mswaki na pia tuendelee kutumia dawa za meno ambazo ni salama kwa afya zetu.

Chanzo: Tanzlife Company Limited

 

About Admin

Avatar

Recommended for you

1 Comment