Articles

UMUHIMU WA DAWA ZA FERROUS PAMOJA NA FOLIC ACID KWA WAJAWAZITO

By

on

Wajawazito ni moja ya makundi pekee katika jamii ambayo yanahitaji uangalizi wa kutosha katika mambo mbalimbali ili kuweza kufanikisha  uzazi salama.

Miongoni mwa mambo ambayo yanahitaji uangalizi na tahadhari kwa upande wa wajawazito ni pamoja na vyakula, vinywaji, matumizi ya dawa, shughuli au kazi za kila siku, kutumia au kuwa katika mazingira ya moshi wa tumbaku/sigara, vilevi na vingine kadha wa kadha. Mambo haya yote huhitaji tahadhari ya kutosha kwa manufaa ya afya ya mama na mtoto pia.

Sambamba na tahadhari zote hizo inashauriwa kwamba, mama anapaswa kuanza kuhudhuria kliniki mara tu ya yeye kujihisi kuwa ni mjamzito.

Madhumuni ya kuanza kuhudhuria kliniki mapema ni pamoja na kufuatilia maendelea ya ukuaji wa mtoto angali bado yupo tumboni lakini pia kufuatilia afya ya mama na kushauri njia bora na salama ili mama asijekupata matatizo wakati wa kujifungua na pia kuweza kupata mtoto ambaye kiafya atakuwa yupo vizuri.

Kwa kuhudhuria kliniki, mama mjamzito atapatiwa huduma mbalimbali kama vile uchunguzi wa sukari mwilini, kiwango cha damu, malaria, magonjwa ya ngono na maambukizi mbalimbali ambayo kwa namna moja ama nyingine yanaweza kuathiri ukuaji wa mtoto pamoja na uzazi salama.

Upungufu wa damu (Anaemia) ni moja ya changamoto ambazo mara nyingi zimekuwa zikijitokeza kwa wajawazito walio wengi. Moja ya sababu ya changamoto hii ni wajawazito kutokuwa na ulaji wa vyakula ambavyo husaidia katika kuongeza kiwango cha damu mwilini. Ikumbukwe kuwa, mwanamke/mama anapopata ujauzito, pia mahitaji ya mwili wake huongezeka na hivyo kulazimu kula vyakula vyenye virutubisho vya kutosha ili kuweza kuijenga afya yake pamoja na mtoto aliyepo tumboni.

Madhara ambayo huweza kujitokeza kwa mama mjamzito kupungukiwa damu ni pamoja na kuathiri ukuaji wa mtoto tumboni, kupelekea mtoto kuzaliwa akiwa na mapungufu katika maumbile/viungo vya mwili, afya ya mzazi kudhoofika na kupata hatari ya kupata magonjwa ya kuambukiza.

Changamoto ya upungufu wa damu ambao umesababishwa na ukosefu wa madini ya chuma katika mwili (Red Blood Cells) hutatuliwa kwa utumiaji wa dawa aina ya Ferrous lakini pia kwa matumizi ya dawa ya Folic Acid ambayo imekuwa ikisaidia katika mgawanyiko wa seli za mwili na kuepusha tatizo la kansa mwilini.

Ferrous na Folic Acid, ni moja ya dawa ambazo hupatikana katika makundi ya virutubisho jamii ya vitamin B.

Katika mwili, umuhimu wa Ferrous na Folic acid ni pamoja na kuongeza madini ya chuma ambayo hutumika katika kuiwezesha damu kubeba na kusafirisha hewa (oxygen and carbon dioxide) ambayo hutumika mwilini/katika damu, husaidia katika kugawanyika kwa seli zinazounda damu mwilini na hivyo kusaidia katika magonjwa ya kansa na pia kusaidia katika kutengenezeka kwa viungo vya mtoto aliyepo tumboni mfano uti wa mgongo.

Dawa hizi zimekuwa zikitolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya (Kliniki za wajawazito) mara tu mjamzito anapoanza mahudhurio yake na kufanyiwa vipimo husika.

Ili kuweza kuwa na mwendelezo mzuri katika lishe na kupata madini haya ya chuma, wajawazito wanashauriwa kutumia vyakula kama vile maini, mboga za majani na nyama ili waweze kupata madini ya chuma na kuongeza damu mwilini. Pia matumizi ya juisi kama vile za Rozela husaidia kuongeza damu mwilini.

Matumizi ya dawa za Ferrous pamoja na Folic Acid yanasaidia katika kuokoa afya za wajawazito pamoja na watoto wachanga. Hii ni njia mojawapo ya kuhakikisha kuwa wanamama/wanawake wanakuwa na uzazi salama na kuepukana na madhara ambayo yanaweza kuleta athari kwa vizaji vijavyo.

Chanzo: Tanzlife Company Limited

 

About Admin

Avatar

Recommended for you