Articles

UMUHIMU WA KUFANYA MAZOEZI KWA WAJAWAZITO

By

on

Mama, na mimi nataka mazoezi!!!.

Mama, na mimi nataka mazoezi!!!.

Kuwa mjamzito, haina maana kwamba ni lazima uwe na uzito mkubwa (mnene) au kuwa umechoka muda wote, bali namna utakavyoonekana kama mama mtarajiwa itategemeana na jinsi unavyojijali kwa upande wa chakula na kuuchangamsha mwili kwa mazoezi.

Ulaji wa vyakula vya aina tofauti tofauti na ufanyaji wa mazoezi, utakuwezesha wewe mjamzito kuwa katika hali nzuri ya kiafya na pia kuufanya mwili uwe imara zaidi.

Mpenzi msomaji, jambo la kuzingatia ni kuhakikisha kabla ya kuanza mazoezi uwe umeonana na daktari wako ili kuona ni mazoezi gani ambayo kwako wewe yatakuwa ni salama zaidi.

Kipindi cha ujauzito, kuna mabadiliko mengi ya muhimu yanayotokea katika mwili. Kama ulikuwa ni mtu wa kufanya mazoezi, ni vizuri ukafanya maboresho katika hayo mazoezi ili yaendane na hali uliyonayo na pia kama ndiyo unaanza kufanya mazoezi, basi jiepushe na mazoezi makali ya ghafla. Kuwa makini na chakula unachokula, nguo unazovaa na aina ya mazoezi unayofanya.

Ili kuweza kufanya mazoezi yenye faida kwako kama mama mjamzito, zingatia vitu vifuatavyo:

Jenga mazoea ya kufanya mazoezi, usifanye au kulazimisha mazoezi magumu ambayo huyawezi. Kumbuka kwamba, unapojenga mazoea ya kufanya mazoezi, usipitishe au kuvuruga utaratibu uliojiwekea wa kufanya mazoezi, kwani kwa kufanya hivyo unapoteza faida ya mazoezi uliyoyafanya awali. ( The Half- Life of Exercise Theory: When more than two and a half days elapse between exercise sessions for the same muscle group, you lose the benefits of the first exercise session ).

Usiendelee kufanya mazoezi wakati unahisi maumivu, zungumza na daktari wako ili kuona namna ya kuboresha mazoezi yako.

Usifanye mazoezi wakati tumbo limejaa chakula, subiri saa moja au moja na nusu baada ya kula chakula ndipo ufanye mazoezi. Kwa kufanya hivyo itakuepusha kuhisi kichefuchefu na hali mbaya tumboni.

Kunywa maji ya kutosha, hata kama hauhisi kiu, kabla, wakati wa mazoezi na baada, itakusaidia mwili usichoke sana na kuondoa sumu mwilini.

Mpenzi msomaji, ni vyema kutoanza mazoezi peke yako endapo unayo mambo yafuatayo katika afya yako, onana kwanza na daktari wako:

Endapo unalo tatizo la kisukari, tatizo la magonjwa ya moyo, tatizo la magonjwa ya mfumo wa upumuaji na pia kama unayo historia ya mimba kutoka au kujifungua kabla ya miezi tisa.

Umuhimu wa kufanya mazoezi siyo tu kwamba unayo faida kwa mama mjamzito, bali pia kwa mtoto aliyeko tumboni.

Tafiti za hivi karibuni zilizofanywa nchini Marekani, zimeonyesha kuwa, mama mjamzito kufanya mazoezi huwezesha mtoto kuzaliwa huku akiwa na ubongo wenye uwezo mzuri zaidi wa kufanya kazi.

Chanzo: Tanzlife Company Limited

 

 

About Admin

Avatar

Recommended for you

1 Comment