Nini maana ya shinikizo la damu, (Blood Pressure) ?
Mishipa hubeba damu na kuisafirisha kutoka kwenye moyo na kuisambaza sehemu mbali mbali za mwili. Mishipa ya kawaida ni laini na rahisi, na damu hutiririka kwa urahisi kupitia hii mishipa. Damu inapotiririka, huweka mgandamizo katika kuta za mishipa, na hili ndilo Shinikizo la damu yako, (Blood Pressure). Shinikizo kubwa la damu ( Hypertension)) hutokea wakati damu yako inatiririka kupitia mishipa yako na kusababisha mgandamizo mkubwa katika kuta za mishipa ya damu, mgandamizo ambao ni mkubwa kuliko ule wa kawaida.
Nini husababisha shinikizo la damu?
Daktari wako anaweza kukusaidia kujua nini kinaweza kuwa chanzo cha wewe kuwa na shinikizo kubwa la damu, vifuatavyo ni baadhi ya vitu ambavyo kwa kawaida vinaweza kusababisha shinikizo la damu kuwa kubwa:
• chakula chenye kiwango kikubwa cha mafuta na hasa mafuta yatokanayo na wanyama, cholesterol
• Mwili kutofanya mazoezi, au kutofanya mazoezi katika kiwango kinachotosheleza,
• Kuwa na uzito mkubwa wa mwili, (overweight)
• Historia ya familia kuwa na shinikizo la damu,
• Matumizi ya tumbaku,
• Msongo wa mawazo, Stress
• Baadhi ya dawa zinazotumika katika kutibu magonjwa
• Matatizo ya figo na homoni.
Kwa nini ni muhimu kupima shinikizo la damu yangu nyumbani na kuweka rekodi yake?
Kupima shinikizo la damu yako nyumbani na kutunza kumbukumbu ya vipimo, huwaonyesha wewe na daktari wako kiasi gani shinikizo la damu yako linavyobadilika au linavyokuwa kila siku. Daktari wako anaweza kutumia rekodi yako ya vipimo kuona jinsi dawa yako inavyofanya kazi ya kudhibiti shinikizo la juu la damu yako. Pia , kupima shinikizo la damu yako mwenyewe ni njia nzuri ya kuchukua hatua katika kusimamia afya yako mwenyewe na kutambua mabadiliko.
Vifaa gani navihitaji katika kupima shinikizo la damu yangu ?
Kupima shinikizo la damu yako nyumbani, unaweza kutumia aidha kifaa cha Digital au Manual, chagua kifaa ambacho kitakidhi mahitaji yako.
Moja ya faida ya kutumia kifaa cha Manual ni kwamba, kinaweza kubebeka kwa urahisi kutoka sehemu moja hadi nyingine, na upande wa gharama yake ni nafuu ukilinganisha na kifaa cha Digital. Utumiaji wake ni mgumu na pia ni rahisi kuharibika na kupelekea kusoma majibu ambayo siyo sahihi.
Kifaa cha Digital ni rahisi kukitumia kwa kuwa kinaonyesha number katika screen, na vipo ambavyo vina karatasi ya kukuwezesha ku-print majibu endapo utahitaji na pia vipo vyenye kuonyesha ishara ya tatizo (Error Indicator) endapo kuna shida imejitokeza katika kifaa. Kifaa hiki ni kizuri pia kutumika hata kwa mtu ambaye ana matatizo ya kusikia kwani hakihitaji kusikiliza mapigo ya moyo. Hasara yake ni kuwa kifaa hiki kinauzwa bei kubwa na kwa kuwa kinatumia betri kinaweza kusoma number au kukupa majibu ambayo siyo sahihi endapo betri au chaji imeisha.
Vitu vya kuangalia/kuzingatia wakati wa kununua kifaa cha kupimia Shinikizo la damu
• Size sahihi, hakikisha unapata size ya cuff (kitambaa) inayoendana na size ya mkono wako. Muulize daktari wako, muuguzi au mfamasia kukuambia ukubwa unao kufaa kulingana na ukubwa wa mkono wako. Shinikizo la damu litasomeka vibaya endapo size ya cuff yako siyo sahihi.
• Iwe na tarakimu ambazo ni rahisi kwako wewe kusoma,
• Kama ni kutumia kifaa cha Manual, lazima uwe na uwezo wa kusikia sauti ya moyo kwa njia hiyo.
• Gharama inaweza kuwa ni sababu muhimu. Gharama kubwa haimaanishi kifaa kitasoma sahihi zaidi.
Nini nahitajika kufanya kabla ya kupima shinikizo la damu yangu?
Baadhi ya mambo ya kuzingatia ni:
• Uwe haujala chakula au kutumia caffeine, pombe, au bidhaa ya tumbaku dakika 30 kabla ya kupima shinikizo la damu yako .
• Pumzika kwa dakika 3 hadi 5 kabla ya kupima shinikizo la damu yako, usifanye majadiliano,
• Weka mkono wako wa kushoto usawa wa moyo wako, juu ya meza au dawati, kaa wima,
• Kutegemeana na aina ya kifaa, pima shinikizo la damu yako.
Nitajuaje kama kifaa changu cha kupimia shinikizo la damu kiko sawa au kama nakitumia vizuri?
Muulize daktari wako, mfamasia au muuguzi akufundishe jinsi ya kutumia kifaa na kupima shinikizo la damu yako kwa usahihi. Matumizi sahihi yatasaidia wewe na daktari wako kufikia matokeo mazuri katika kudhibiti shinikizo la damu yako.
Je, shinikizo la damu yangu maana yake ni ipi?
Daktari wako anaweza kukuambia kama una shinikizo la juu la damu. Madaktari wengi huangalia shinikizo la damu yako mara kadhaa kwa siku tofauti kabla ya kuamua kwamba una shinikizo la juu la damu. Kama una shinikizo la juu la damu, unahitaji kuangalia shinikizo la damu yako mara kwa mara na kuendelea kuwasiliana na daktari wako.
Kama una ugonjwa wa kisukari au ugonjwa wa figo , shinikizo la damu yako linaweza kuwa chini zaidi kuliko watu wengine. Zungumza na daktari wako kujua ni wakati gani wewe unahesabika kuwa una shinikizo kubwa la damu.
Kwa kawaida Shinikizo la damu huwa ni 120/80, na kuanzia 140/90 na zaidi huhesabika kuwa ni shinikizo kubwa la damu (Hypertension), chini ya 90 au pointi 25 chini ya Shinikizo la damu yako la kawaida huhesabika kuwa wewe una Hypotension yaani Shinikizo la damu yako lipo chini.
Chanzo: Tanzlife Company Limited