Articles

YAJUE MAISHA NA SIRI YA VIRUSI KUTOTIBIKA KIRAHISI

By

on

VIRUSI

VIRUSI

Maisha ya viumbe hai na binadamu kwa ujumla siku zote kiafya kuna, magonjwa na pia kuna uzima (afya bora). Katika magonjwa yapo yasiyosababishwa na vijidudu na yapo yale yanasosababishwa na vijidudu.

Vijidudu visababishavyo magonjwa ( nitazungumzia kwa binadamu ) vipo vya aina tofauti tofauti, mfano wake ni makundi ya wadudu jamii ya bacteria, fangasi pamoja na virusi. Makundi haya ya vijidudu ingawaje yote husababisha magonjwa kwa binadamu lakini kuna utofauti mkubwa sana miongoni mwa makundi haya ikiwa ni tofauti za kitabia na hata kimaumbile.

Mpenzi msomaji, leo tutaangalia kundi hili la wadudu jamii ya VIRUSI ambalo ndilo linalosababisha magonjwa mengi hatari mfano Ebola, Ukimwi, Dengue na mengine mengi.

Kikawaida wengi wetu tunafahamu ya kuwa, unapozungumza neno viumbe au kiumbe, basi kuna mambo mawili, aidha ni kiumbe HAI au ni kiumbe ambacho SIYO HAI. Jambo linalotuwezesha kufahamu kuwa kiumbe hiki ni hai au siyo hai ni sifa ambazo kiumbe husika kinakuwanazo, mfano tunaposema kiumbe ni hai basi kitakuwa na sifa zifuatazo, uwezo wa kuzaliana, kukua, kutoa taka mwilini, upumuaji, ulaji chakula, kujongea pamoja na kuwa na uwezo wa kuhisi kile kinachotokea katika mazingira. Endapo kiumbe hakitakuwa na sifa hizo basi kiumbe hicho kitahesabika kuwa SIYO HAI.

Tofauti na ilivyo kwa viumbe wengine, maisha ya virusi yanaweza kuwekwa katika makundi yote mawili, yaani unaweza kumuweka katika kundi la viumbe hai na pia unaweza kumuweka katika kundi la viumbe ambavyo SIYO HAI, na hapa ndipo ugumu unakuwepo katika kumdhibiti kiumbe huyu hususani inapofika wakati wa kutibu na kuzuia magonjwa yasababishwayo na virusi.

Virusi vinapokuwa nje ya kiumbe mwingine ( kwa kitaalam, host ) huhesabika kama kiumbe kisichokuwa hai, kinakuwa ni sawa na unavyoona jiwe, kwani haviwezi kuzaliana, kukua au kufanya chochote kile kinachoweza kufanywa na kiumbe hai, ila vinapopata nafasi ya kuingia katika mfumo wa kiumbe mwingine mfano katika damu, basi hapo virusi hao huanza maisha yao upya. Mfano virusi vinavyosababisha ugonjwa wa ukimwi, vikiwa nje ya mwili wa binadamu, havitaweza kuzaliana wala kukua, vitakaa mahala pake kama ni katika nyembe, sindano au popote pale, vitakuwa kama vumbi au jiwe, na endapo vitapata nafasi ya kuingia katika damu, maisha yake yataanza upya. Ndani ya binadamu watazaliana, kukua na kufanya kila kitu kama viumbe wengine walio hai. Sifa hii ni tofauti kwa viumbe wengine ambao wao hawawezi kujumuishwa katika makundi yote mawili ya viumbe hai na visivyo hai.

Kutokana na virusi kuwa na sifa zote mbili, za viumbe hai na visivyo hai, imechangia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza ugumu wa kupambana na magonjwa yasababishwayo na vijidudu hivi mfano, Ukimwi na Ebola, ikiwa ni katika ugumu wa kupata dawa za kuzuia na kutibu. 

Chanzo: Tanzlife Company Limited

About Admin

Avatar

Recommended for you