Chumvi ni kiungo ambacho kimekuwa kinatumiwa na mwanadamu tangu enzi na enzi katika kuongeza ladha ya vyakula mbalimbali na kumfanya mlaji wa chakula akile katika ladha aipendayo.
Pamoja na kuwa chumvi huongeza ladha katika chakula, mpenzi msomaji tukumbushane vitu muhimu vinavyoifanya chumvi iitwe chumvi: Chumvi tuitumiayo katika vyakula ( Table salt ) ni muunganiko wa madini haya, sodium pamoja na chloride ambapo kwa kitaalamu zaidi chumvi huitwa na kuandikwa hivi, sodium chloride (Nacl).
Mpenzi msomaji, utaona kwamba, chumvi siyo tu humpatia mtu ladha ya chakula, bali ni sehemu mojawapo ya kumuongezea mtu madini muhimu ya kuufanya mwili wake ufanye kazi vizuri zaidi, mfano baadhi ya kazi za madini ya sodium ni kuusaidia mwili katika kusafirisha taarifa mbali mbali kutoka sehemu moja hadi nyingine katika mwili, pia madini haya huuwezesha mwili kuhifadhi maji kutegemeana na mahitaji ya mwili.
Kupitia chumvi, pia imekuwa ni njia mojawapo ya kumuwezesha mwanadamu apate madini haya ambayo kwa namna moja au nyingine mtu hawezi kuyapata kupitia vyakula anavyokula kila siku, mfano mzuri ni madini ya joto ambayo kwa kitaalamu huitwa Iodine, madini haya huongezwa katika chumvi ili kumuwezesha mlaji ayapate na yamuwezeshe mfumo wake wa homoni ( Thyroid gland ) ufanye kazi vizuri. Binadamu akiyakosa madini haya ya Iodine au madini joto hupatwa na ugonjwa uitwao goita, ambapo moja ya dalili zake ni kutokea uvimbe eneo la kooni.
Mpenzi msomaji, wenzetu husema kwamba, „everything too much is harmful” wakiwa na maana kwamba, kila kitu au jambo linapofanyika kupita kiasi, basi huwa na madhara. Vivyo hivyo, endapo mtu ataitumia chumvi katika kiwango kikubwa zaidi, basi mtu huyu atapata madhara kiafya.
Madhara ya kiafya yatokanayo na ulaji wa chumvi kupita kiasi ni pamoja na kuathirika kwa mfumo wa mawasiliano katika mwili na pia kutokana na chumvi kuwa nyingi mwilini, mwili utajikuta unahifadhi maji mengi zaidi kupita kawaida na hii hufanyika kupitia figo ambazo katika mwili baada ya chumvi kuzidi, zenyewe huruhusu maji mengi yabaki mwilini kwani chumvi huyavuta maji haya na matokeo yake maji haya huingia katika mfumo wa damu, maji mengi yakiingia katika mfumo wa damu hupelekea ujazo wa damu uongezeke, madhara yatokanayo na kuongezeka kwa ujazo wa damu ni kuongezeka kwa shinikizo la damu ( high blood pressure ).
Utaona kwamba, ulaji wa chumvi nyingi hupelekea mtu apate ugonjwa wa moyo au kuwa na shinikizo kubwa la damu, na tatizo la kuwa na shinikizo kubwa la damu husababisha mtu apate matatizo mengine ambayo hakuyategemea mfano matatizo katika uwezo wa kuona, matatizo ya figo, kuhisi ganzi mwilini pamoja na hatari ya kupata kiharusi.
Kiwango cha chumvi ambacho mtu anapaswa kukitumia kwa siku ili asipate madhara yoyote yatokanayo na wingi wa chumvi mwilini ni robo tatu ya kijiko cha chai sawa na gramu mbili kwa siku ( 2gm per day ).
Mpenzi msomaji, jihadhari na hatari ya kupata shinikizo kubwa la damu kwa kuzingatia kiwango cha chumvi unachopaswa kula kwa siku.
Chanzo: Tanzlife Company Limited
Pingback: ZIFAHAMU ATHARI ZITOKANAZO NA ULAJI WA CHUMVI NYINGI | Blog Mama